Mungu kwanza

Monday 20 May 2024

NGUVU YA KUACHILIA NA KUSAMEHE

 



Lengo la somo:

Kumuelekeza Mkristo juu ya umuhimu wa kusamehe na kuachilia, na jinsi kitendo hiki kinavyoleta amani na uhuru katika maisha ya mwamini(Mkristo).

Sehemu ya Kwanza: Utangulizi

  1. Maana ya Kusamehe na Kuachilia:

    • Kusamehe: Kusamehe ni tendo la kuachilia hasira, kinyongo, na uchungu dhidi ya mtu aliyekukosea. Ni kuchukua hatua ya kimakusudi ya kuruhusu amani ya Mungu itawale moyo wako badala ya uchungu na hasira.
    • Kuachilia: Kuachilia ni kitendo cha kutoweka shinikizo au mizigo ya kiroho na kihisia inayotokana na makosa ya wengine. Ni pale unapomwachia Mungu mzigo wa adhabu na haki, ukimwomba akusaidie usiwe na kisasi au chuki moyoni.
  2. Umuhimu wa Kusamehe:

    • Kusamehe ni amri ya Mungu. Katika Mathayo 6:14-15, Yesu anasema, "Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, na Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu."
    • Kusamehe huleta amani na uhuru wa ndani(moyo). Uchungu na hasira vinapondolewa, moyo unaanza kujawa na amani na furaha ya kweli.
    • Kusamehe huondoa mizigo ya kiroho na kihisia ambayo inaweza kuathiri maisha ya kila siku. Uchungu na kinyongo vinaweza kusababisha matatizo ya afya kama vile shinikizo la damu, matatizo ya moyo, na msongo wa mawazo.

Sehemu ya Pili: Misingi ya Kibiblia kuhusu Kusamehe na Kuachilia

  1. Mfano wa Yesu Kristo:

    • Yesu alitufundisha kusamehe kupitia mfano wake wa maisha. Akiwa msalabani, aliomba kwa ajili ya watesi wake, akisema, "Baba, wasamehe, kwa maana hawajui watendalo" (Luka 23:34). Huu ni mfano wa hali ya juu wa msamaha usio na masharti.
  2. Mathayo 18:21-22:

    • Petro alimuuliza Yesu ni mara ngapi anapaswa kumsamehe ndugu yake, na Yesu akajibu, “Si mara saba, bali hata saba mara sabini,” akisisitiza kuwa msamaha hauna kikomo. Hii inaonyesha kuwa msamaha unatakiwa kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
  3. Mathayo 6:14-15:

    • Yesu alifundisha kwamba kama hatutasamehe wengine, Baba yetu wa mbinguni hatatusamehe dhambi zetu. Hii inaonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya kusamehe na msamaha wa Mungu kwetu.
  4. Waefeso 4:32:

    • “Iweni wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu alivyowasamehe ninyi katika Kristo.” Hii inaonyesha kuwa tunapaswa kuwa na huruma kama Mungu alivyokuwa na huruma kwetu, na kusamehe kama tulivyopokea msamaha wake.
  5. Wakolosai 3:13:

    • “Vumilianeni na kusameheana. Kila mtu anayeona ana sababu ya kumlaumu mwenzake, kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi, ndivyo na ninyi mnavyopaswa kusamehe.” Hii inaonyesha kuwa kusamehe ni agizo na si chaguo, na tunapaswa kufanya hivyo kwa uvumilivu na upendo.

Sehemu ya Tatu: Matokeo Chanya ya Kusamehe na Kuachilia

  1. Amani na Utulivu wa Moyo:

    • Kusamehe kunaleta amani ya ndani na kupunguza mizigo ya kihisia (Filipi 4:6-7). Unapomsamehe mtu, unaachilia mzigo ambao ulikuwa unakufanya usiwe na amani. Kwa kuachilia huo mzigo, unapata utulivu wa moyo na amani ya kweli kutoka kwa Mungu.
  2. Mahusiano Bora na Watu:

    • Kusamehe kunajenga na kuimarisha mahusiano na wengine, huondoa kinyongo na chuki (Warumi 12:18). Mahusiano yanaimarika kwa sababu hakuna chuki na kinyongo kinachokwamisha mawasiliano na uhusiano mzuri.
  3. Afya ya Mwili na Akili:

    • Utafiti umeonyesha kuwa kusamehe kunachangia kuboresha afya ya mwili na akili kwa kupunguza msongo wa mawazo na magonjwa yanayohusiana na moyo. Uchungu na hasira vinaweza kusababisha matatizo ya kiafya, lakini kusamehe kunasaidia kuondoa vyanzo vya matatizo hayo.
  4. Kusamehe kunavuta baraka za Mungu kuja kwako:

    • Kusamehe kunafungua mlango wa baraka na kibali cha Mungu katika maisha yetu (Mathayo 5:7). Mungu anabariki wale wanaotii amri zake, na kusamehe ni mojawapo ya amri hizo.

Sehemu ya Nne: Changamoto na Jinsi ya Kushinda

  1. Kushinda Uchungu na Hasira:

    • Ni muhimu kumwomba Mungu msaada kwa maombi (Zaburi 51:10). Omba Mungu akupe moyo safi na upyae roho iliyoinama. Kuomba msaada wa Mungu kunasaidia kushinda uchungu na hasira zinazotokana na makosa ya wengine.
    • Kutafakari na kujaza mawazo chanya kutoka kwa Neno la Mungu. Soma na kutafakari maandiko yanayozungumzia kusamehe na upendo wa Mungu, ili ujaze mawazo yako na mambo chanya.
  2. Kutafuta Msaada wa Kiroho:

    • Ushirika na watu wa Mungu ambao wanaweza kusaidia kwa ushauri na maombi (Yakobo 5:16). Kushirikiana na waumini wengine ambao wanaweza kutoa msaada wa kiroho na kukutia moyo katika safari yako ya kusamehe.
  3. Kufahamu Wema na Huruma ya Mungu:

    • Kutambua jinsi Mungu alivyo mwenye rehema na anatupenda bila masharti (Zaburi 103:12). Kuelewa kwamba Mungu ametusamehe makosa yetu yote, na anatupenda bila masharti, kunatusaidia kuona umuhimu wa kusamehe wengine.

Sehemu ya Tano: Hitimisho

  1. Kufanya Maamuzi:

    • Mkristo achukue hatua ya kusamehe na kuachilia mizigo yake leo. Afanye maamuzi ya dhati ya kuachilia hasira, uchungu, na kinyongo.
    • Kuwa na nidhamu ya kila siku ya kutafakari Neno la Mungu na kuomba msaada wa Roho Mtakatifu. Nidhamu hii itasaidia kuendelea katika safari ya kusamehe.
  2. Maombi ya Pamoja:

    • Omba pamoja ili Mungu atoe nguvu na uwezo wa kusamehe kutoka moyoni. Maombi ya pamoja yana nguvu na yanaweza kusaidia kuleta mabadiliko ya kweli.

Rejea za Biblia:

  • Mathayo 6:14-15
  • Mathayo 18:21-22
  • Luka 23:34
  • Waefeso 4:32
  • Wakolosai 3:13
  • Warumi 12:18
  • Filipi 4:6-7
  • Zaburi 51:10
  • Yakobo 5:16
  • Zaburi 103:12
  • Mathayo 5:7

Maelezo Mafupi Juu ya kusamehe na Kuachilia

Luk 17:3-4 Kisha Petro akamwendea Yesu akamwambia ‘Ndugu yangu anikose mara ngapi nimsamehe? Hata mara saba?

Kutosamehe kunachafua roho yako, unaweza kuikosa Mbingu au Baraka za Mungu.

Malaika ni wajumbe, watumishi wa Mungu wanapotumwa kwako kukuletea mahitaji mbali mbali sababu wenyewe wapo katika roho wanapo kuja wanaiona roho yako imechafuka basi wanarudisha kile kitu walichokuletea wanaenda kukihifadhi kinakaa kilipotolewa, kwa duniani hifadhi hizo tungeweza kuiita kabati, friji, store mpaka utakapo kaa sawa sawa etc.

Mungu hawasikilizi wenye dhambi maombi (Yoh mt 9:31) , sifa zao kwa Mungu huonekana kama ni makelele.

Migogoro mingi katika ndoa chanzo kikubwa ni kutosameana Mume, mke, mtoto mabubu mhhhhh.Kunyimana nyimana vitu vilivyo haki katika ndoa, kukomoana. Mwanamke& Mwanaume kunyemelewa na Shetani kuhusu kutafuta altenative ( Mpumbavu huamua fasta, madhara yakamkuta) Shetani anazunguka zunguka akitafuta mtu, mwanachama ajoin, mapepo nayo yanazunguka zunguka hayalali. (1Pet 5:8)

Mit. 17: 22, Moyo uliochangamka ni dawa nzuri;Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.

Baadhi ya Matatizo/ athari anazoweza kupata mtu aliye na roho ya kutosamehe/Uchungu wa Moyoni

Mioyo yetu haikuumbwa ikae na uchungu, hasira, chuki. Ukikaribisha vitu hivyo unakaribisha Magonjwa, k.v. Presha, Kichwa Kuuma, Vidonda vya Tumbo, Kuchanganyikiwa (Kuongea Peke yako),  Ajari, Asilimia kubwa ya watu wanojinyonga, kunywa sumu ni watu walioumizwa na uchungu uliopitiliza

(Yuda Iskariote Mt 27:5), Watu wengine wamekasirika wakaijikuta wapo Kifungoni wanajuta.Petro hakuwekeza kosa alilotenda la kumkana Yesu tena mara 3 alitubu nakuomba msamaha, Akasamehewa.

 Sala Ya Bwana Tunakiri kuwa “Baba yetu uliye Mbinguni, utusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe Waliotukosea” Tunajifunga kwa maneno ya kinywa chetu wenyewe. Kama hutaki kusamehe na kuachilia na Mungu naye hakusamehi ng’o nani anayeweza kuishi bila msaada wa Mungu, bila ulinzi wake, upendo wake, neema yake? Ukihukumiwa kwa kosa hilo siku ya siku ni haki yako sababu umekiri kwa kinywa chako mwenyewe.

Tuwe wepesi wa kuomba msamaha kwa Mungu wetu, wenzi wetu hata watoto wetu

Katika wanafunzi aliokuwa nao Yesu Yuda alimsaliti Yesu akakaa na uchungu hakuutoa ukamdhuru , Petro naye alimsaliti Yesu tena mara tatu. Yuda mara moja, Petro mara tatu akatubu fasta. Akapata msamaha, sio suala la dhambi kubwa au ndogo Mungu kwake hata dhambi iwe nyekundu husamehe kabisa.

 Stephano Alipigwa na vijana waliofundishwa na Sauli Stephano” Alikufa huku akiomba Bwana Usiwahesabiae Dhambi hii, wasamehe Bwana.

Bwana Yesu pamoja na kudhalilishwa yeye akiwa kama Mwana wa Mungu alikuwa na Jeshi kubwa la Malaika ambalo angeweza kuliamlisha lifanye vyovyote, likafanya alidhalilishwa lakini akasema, Bwana wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.

Eliya alifanyaje ? Kama Eliya aliweza kuagiza moto kutoka Mbinguni uteketeze 50 Yesu si Zaidi! Eliya Mtu wa Mungu kama mimi, kama wewe tu. Aliweza Yesu JE ! 2 Wafalme 1:10

Kutoomba Toba na kiburi mbele za Mungu au wanadamu, maandiko yanasema Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa neema wanyenyekevu.

Sio kwa sababu maandiko yanasema Samehe saba mara sabini basi ndo iwe tiketi ya  wewe kukosea kwa makusudi , sababu utasamehewa kwa hiyo ukaamua kuleta Makwazo ya makusudi. Maandiko yana onya juu ya mtu kama huyo alitaye makwazo. Pia sio kwa sababu Mungu ni wa huruma au anasemehe si mwingi wa hasira, tusijiachilie sana tuwe na taadhali.

Luka 17.1 Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!

Waefeso 4:26-27 '' Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na ...

Shetani hawezi kukushambulia mpaka umfunguliae Mlango hasira ni Mlango mmojawapo anaotumia

Kisasi ni cha Mungu, yeye atalipa tena walkati mwingine Mungu hulipa tangia hapa duniani, Duniani tunapita hatuishi milele

Abigaili, mwanamke mwenye hekima wa Israeli la kale, anatuwekea kielelezo kinachoonyesha matokeo ya kuomba msamaha, ingawa aliomba msamaha kwa kosa la mumewe. Alipokuwa akiishi nyikani pamoja na watumishi wake, Daudi, aliyekuja kuwa mfalme wa Israeli, alilinda kondoo za Nabali, mume wa Abigaili. Hata hivyo, wakati vijana hao wa Daudi walipoomba mkate na maji, Nabali aliwafukuza na kuwatusi vibaya sana.

Daudi alikasirika na kuongoza wanaume 400 hivi kwenda kumpiga Nabali na nyumba yake. Alipojua habari hiyo, Abigaili alifunga safari kwenda kumlaki Daudi. Alipomwona, Abigaili alimwangukia miguuni pake na kusema: “Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.” Kisha Abigaili akaeleza hali ilivyokuwa na kumpa Daudi zawadi ya chakula na maji.

Ndipo Daudi akamwambia: “Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.” 1 Samweli 25:2-35. Baada ya siku 10 Nabali alifariki, alivyofariki Daudi alifanya mpango wa kumuoa Abigaili (Malipo ni hapa hapa Duniani)

Solomoni Mukubwa (Ushuhuda)

Yeye ni Raia wa Kongo anayeishi Kenya ni mtoto wa kwanza katika familia yao baba yao alipoongeza mke mwingine Huyo mke Mwingine alimloga Solomoni Mukubwa alipokuwa na umli wa Miaka 12 akawa na uvimbe ambao ulipelekea kukatwa kwa mkono wake ili kunusuru uhai wake, aliangaikiwa sehemu nyingi na wazazi wake bila mafanikio.

Alijua kuwa amelogwa na mama yake wa kambo baada ya yeye mwenyewe kukiri kuwa alifanya hivyo. Huyu mama wa kambo naye aliokoka baada ya yeye naye kupata pigo ‘Mwanawe alirukiwa na kijiti cha moto jichoni kilichopelekea jicho la mwanawe kuharibika kabisa

(Malipo ni  hapa hapa Duniani)  ameimba wimbo unaitwa nimewasamehe !!!

Usipende kuudhi watu ovyo ovyo watu wengine Wanampendeza Mungu kiasi ambacho ukikorofishana nao Malaika wananunua ugomvi unashangaa tu, unapata pigo hujui chanzo ni nini.Hata katika ufalme wa giza nao kama kuna kufanana Fulani ukimfanyia kitu kibaya anayelindwa na majini unaweza kukuta majini wanakushambulia hata kukuua kabisa.

Kaini na Habili

Kisa cha Kaini kumuua Habiri ni hasira, uchungu ambao haukutubiwa Mwanzo 4:1-15

uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.(Waefeso 4:31,32)

Mwisho wa Somo:

Mkristo anahimizwa kuanza safari ya kusamehe na kuachilia, akijua kuwa kwa kufanya hivyo anamfuata Kristo na kupokea baraka zake za amani, furaha, na uhuru wa kweli. Kusamehe ni njia ya kuleta uponyaji wa ndani na kuishi maisha yenye furaha na amani.


Classified Mindsets

Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428