Mungu kwanza

Friday, 22 June 2018

TUNDA LA MTI WA UJUZI WA MEMA NA MABAYA.

Agizo ni lile, mti wa ujuzi wa mema na mabaya una matunda au una tunda ambalo Adam na Eva walipokula hawakubaki salama na hawakubaki vile walivyokuwa. Hii imemaanisha kuwa kila mtu anayo fursa ya kupatia na kukosea kila sekunde ya maisha yake kwasababu ndani yake ana kiwango cha ujuzi wa mema na mabaya. Kiwango hiki cha ujuzi wa mema na mabaya ni matokeo ya kula tunda la mti huu, kosa ambalo tumelirithi toka kwa Adam na Eva, kosa la kutokutii neno la Mungu.

Mti wa ujuzi wa mema na mabaya ulibeba maarifa na ufahamu wenye pande zote mbili yaani wema na ubaya. Matunda ya mti huu Mungu aliwakataza Adam na mkewe kwamba wasile maana hakutaka wajue mema na mabaya. Mungu alitaka tujue mema tu, hakutaka tujue mema na mabaya. Katikati yake hapo kulitakiwa *UTII*. Kutii agizo la Mungu au kuukubali ushawishi wa shetani ndani ya nyoka. Kwa bahati mbaya sana, Adam alichagua kumtii nyoka na kupotelea kwenye DUNIA ILIYOPOTEA.

*Kula matunda ya mti huu wa ujuzi wa mema na mabaya ni kuelewa na kukubaliana na kuamini na kutekeleza maarifa na ufahamu uliokuwa umebeba ujuzi wa mema na mabaya.* Wema wa muonekano na kule kuvutia na kutamanika kwa chakula na kupendeza kwa macho na kupata ufahamu zaidi. Ubaya wa uharibifu uliojificha ndani ya kutokumtii Mungu na madhara yake yote kwa ujumla. Yaani kujua mema na mabaya halafu unajikuta kila ukitaka kutenda mema unashindwa na kukuta umetenda mabaya tu.

Unajua kuomba ni jambo zuri na jema na sahihi ila unajikuta hujaomba na badala yake umeangalia movie masaa 6 na unaanza kujishangaa kwanini jema ulilotaka kulifanya hujalifanya na badala yake umetenda baya ambalo hulitaki. Ni fumbo kubwa hili na ndio maana *hakuna mwanadamu anaweza kuishinda dhambi kwa nguvu zake mwenyewe au kwa elimu au pesa au umaarufu wake. Bila msaada wa Mungu kwa ROHO MTAKATIFU katika Kristo Yesu, hali zetu ni mbaya sana*. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, hata dhambi zenyewe, ukute ni dhambi kweli ila unaipenda, utaishindaje? Wakati moyoni mwako unaitaka, mwili una shauku. Ni rahisi kwa kiwango gani kuishinda dhambi unayoipenda?

Mti huu ni ufahamu, yale maarifa ambayo ndani yake yalibeba ujuzi wa mema na mabaya, sio mema au mabaya. Hii inamaanisha yote mawili yapo pamoja. Ni kitu kigumu sana kukipatia picha. Ila fikiri biblia inasema shetani anaweza kujigeuza na kuwa malaika wa nuru. Hivyo anaweza kujigeuza kuwa mwema lakini kiasili na kimsingi na kihatma ni mbaya. Biblia inasema shetani ni BABA WA UONGO, hana ukweli wowote na hawezi kusema ukweli. Akisema uongo unaofanana na ukweli bado sio ukweli kwani uongo kwa asilimia 99 bado ni uongo tu.

Ndio maana lazima tufanye bidii kutofautisha kanuni za kupima ubora na usahihi wa TAARIFA ambazo tunazipata kila siku na hasa ukizingatia kuwa MAMBO MENGI YAMETENGENEZWA. Ili ujue kuwa umaarufu sio kipimo cha usahihi kwa kiwango ambacho utakubali kuwa UZURI SIO USAHIHI NA UBAYA SIO KUTOKUWA SAHIHI. Yako mazuri mabaya na mabaya mazuri mpaka tunafika mahali tunachanganyikiwa hatujui nini ni nini. Na hii ndio inayosema ule umuhimu wa KUMTEGEMEA SANA ROHO MTAKATIFU maana yeye anaijua KWELI YOTE na yuko tayari kutuongoza.

Mwanzo 2:16-17
BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani, [Mwa 3:11, 17; 9:29; Yer 42:16; Kum 30:15, 19; Eze 3:18; Rum 5:13; 6:23] lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”

Mwanzo 3:4 Yn 8:44; 2Kor 11:3
Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika" hamtakufa.

Ndio sasa tunahangaika na hiyo HAKIKA. Hakika moja; ni ya Mungu. Hakika nyingine ni ya shetani.
Chaguo ni lako na langu. MATUNDA YA MTI WA UZIMA.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428