Mungu kwanza

Saturday, 30 December 2017

MTEGO HUTEGWA BURE MBELE YA MACHO YA NDEGE YEYOTE




         MTEGO HUTEGWA BURE MBELE YA MACHO YA NDEGE YEYOTE

Jesus Up!-Mithali 1:1-33


Kwakuwa mtego hutegwa bure, mbele ya macho ya ndege yeyote na kila ndege anayo nafasi ya kutegeka na kujiangamiza nafsi yake maana hakuna ndege aliyebembelezwa kufika kwenye mtego. Hebu fikiri panya. Unapotega mtego wa panya ni lazima uweke kitu cha kumvutia ili aipeleke nafsi yake katika uharibifu kwa kipande cha nyama, laiti kama panya angejua kuwa kadri anavyousogelea mtego ndivyo siku zake za kuishi zinavyopungua. Mitego mingi huwa inavutia sana na hakika huwezi kuona kama ni wewe ndo unategwa kwani hata ndege na panya huwa wanajishangaa sana wakijikutana wamenaswa na sasa wanasubiria mauti yao. Unapomtega ndege hata ikiwa ni kwa ulimbo ni lazima utaweka mazingira ya kumshawishi ili asogee karibu zaidi na mtego na kisha ashindwe kabisa kutoka. Kama ulishavua samaki kwa ndoano kama mimi utaelewa ninachokisema kuwa mtego hutegwa bure mbele ya macho ya kila samaki na samaki atakaefanikiwa kuuna na ukamvutia na kuufuata basi ni lazima yeye atapatikana kama kitoweo. Lakini hata kwa ndoano kuna kitu tunaita chambo, chambo ni aina ya udanganyifu wa kitu kinachovutia machoni pa samaki au ndege au panya ambacho akikiona anapoteza ufahamu wa kugundua kuwa hiyo chambo imevikwa juu ya ndoano au sumu na samaki atakimbilia katika mauti yake kwa kipande cha chambo. Uzuri wa mtego ni kwamba ni mtego.

Uzuri wa mtego ndo huo, ni mtego kwake anaetegwa na zipo sababu nyuma ya kila mtego na nataka niseme kidogo hapo. Kila mtego unategwa kwa sababu maalum kabisa, yaani sababu mahususi ya kupata anaetafutwa aidha kwa kuliwa kama samaki na ndege au kwa kuondolewa eneo husika kama panya vile. Wachache hutega panya kwa kumla ila samaki na ndege ni kwa chakula hakika. Ndo nasema kila mtego una sababu ya kwanini umetengenezwa, kwanini umetegwa na kwanini umetegwa muda huu na kwanini umetegwa mahali hapo. huwezi ukatega mtego mahali ambapo unajua hakuna ndege, kwahiyo mtego wa panya lazima uwekwe kwenye LOCATION ambayo panya wamezoea kutembelea katika shughuli zao za uharibifu. Kila mtego hutegwa kwa kuzingatia muda ambao mtegwa atapata fursa ya kujipeleka na ndio maana mitego mingi ya panya ni usiku kama ambavyo huwezi kutembea barabarani umevaa chandarua kwa kumkwepa mbu. Mtego wa panya sio lazima ushike samaki maana samaki ni tofauti sana na ndege na kila mmoja anashikwa kwa mtego wa aina yake. Ni ukweli kwamba mtego unapotegwa, mtegaji anachotaka ni kupata kitu na kwenye hicho kitu anachotaka basi ni lazima awe mlengwa,yaani ikitokea mtego wa panya umemkamata samaki basi samaki atakuwa amejipendekeza na kwanza ilikuwaje akatoka kwenye maji? Matarajio ni kwamba mtego wa ndoano itakamata samaki na mtego wa panya utakamata panya na ndege nae atanaswa kwenye ulimbo.

Kuna cha zaidi cha kujua kuhusu hili jambo, sio kila mtego huwa unaleta kinachotazamiwa kwani zipo sababu nyingi za kuhakikisha ndoano imemkamata samaki na mojawapo ni, huenda umetupia ndoani mahali ambapo samaki wamehama na au wapo walini wameshiba na au wamegundua kuwa wanategwa na kwa hiyo wamejifunza kula chambo pasipo kumeza ndoano nzima. Hao ni viumbe wasio na utashi kama binadamu. Kwanini nimechukua muda wote huu kuelezea kuhusu mtego, ni kwasababu ni rahisi zaidi kumtega kijana kuliko panya. Nitaelezea.


NGUVU YA USHAWISHI YA WENYE DHAMBI
Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe Usikubali. Maisha ya vijana wamezungukwa na ushawishi wa mambo mengi sana mazuri na mabaya na kwakweli mabaya yanaonekana kupata nguvu zaidi kuliko mazuri. Vijana wamezungukwa na watu wabaya na wazuri na inaonekana kana kwamba watu wabaya wanapata fursa zaidi kuliko wema ndani ya nafsi ya kijana. Na ndo maana ukifanya tathimini yakow ewe kama kijana utaona asilimia kubwa ya makosa ulofanya yalikuwa ni matokea ya kumuamini mtu asiyeaminika yaani kujitega kwenye mtego wako mwenyewe kwa faida ya maisha yako. Na ndio maana utaona wale waovu na wenye dhambi wamekuwa wakitumia udanganyifu wa mali na vitu vinavyoonekana vizuri kwa macho au pesa, simu za mkononi: kwa ujumla tamaa za mali na shughuli za dunia hii zimewakosesha vijana wengi sana,na wengine hata hawakuendelea kuishi baada ya kuingia mtegoni. Wameshawishiwa na vitu vinavyomeremeta na kung’aa kuliko almasi na wengine wanazo sababu nzuri sana za kukosea na huo ndio uzuri wa mtego.

Wengine walilipiwa ada kwasababu wanasema wazazi wao hawana uwezo na huku hawajui kuwa kutokuwa na uwezo sio umasikini maana tatizo la ada sio la kudumu bali wengi sana wametumia mbinu ya kudumu kutatua matatizo ya muda mfupi na kuharibu maisha yao. Na kumbe tatizo sio tatizo lenyewe ila mwenye tatizo na namna anavyotaka kulibeba tatizo ili ajisikie vizuri. Wapo masikini na watu wasio na uwezo lakini hawakushusha utu wao kwa pesa, na kwa wakaka utakuta wengi sana wamekuwa mashoga au wamebebwa na masukari mama ili watunzwe na wengi husema ndo maisha ya mjini hayo. Hakuna sababu nzuri ya kukosea. Hakuna sababu nzuri ya kuharibu maana kwenye kila sababu utakayotoa kuna watu walivuka bila kukosea na wewe unaweza ukadhani uko peke yako dunia nzima mwenye tatizo lakini kimsingi ni vile hujajua, kumbuka kutokujua hakuondoa uwepo wa kitu mahali isipokuwa kwenye ufahamu wa mjinga mwenyewe. Sio kila anaekosea anakosea kwasababu ana shida, Eva hakula tunda kwasababu aklikuwa na njaa ila Esau aliuza haki ya uzaliwa wa kwanza kwasababu ya njaa na huku Daniel na wenzake walikataa kula chakula cha mfalme ili wasijitie unajisi. Eva alishawishiwa kama ambavyo shetani alimshawishi Yesu alipokuwa na njaa. Nguvu ya ushawishi wa mwenye dhambi iko ndani ya uzuri wa jambo analolileta kwako n ahata kama likikuwa baya basi wewe kama hauko vizuri unaweza kuona ni sawa na kumbe ndio uharibifu wako umefika. Muulize samaki na chambo au panya na kipande cha nyama.


Kipande cha nyama kinachonukia kinatosha kumkamata panya na kuondoa uhai wake hapo inategemea sana kama panya akiona ni kipande cha nyama peke yake. Sio lazima panya ale kile kipande ndo ashikwe na tena sio panya wote wanashikwa kwakuwa walikula, hapana. Kumbuka huu ni mtego, una kitu cha siri pia ambacho panya atakijua akishakamatwa. Kumbe kile kipande ndo mtego wenyewe maana ndoano haina nguvu ikiwa peke yake na wala haimvutii samaki na ndio maana ukitaka ukeshe ukivua samaki bila kupata basi nenda kavue samaki kwa ndoano bila chambo. Huwezi pata kitu. Unadhani rafiki yako angekwambia kuwa jambo analokushawishi kulifanya lina madhara ungekubali kwenda nae? Alivyokwambia hawezi kununua mbuzi kwenye gunia na wewe ukakubali ngono kabla ya ndoa ulikuwa hujui kuwa sio lazima ununue mbuzi kwenye gunia? Ulipoambiwa uuthibitishe upendo wako kwake kwa kuvua nguo zako zote kama kichaa tena mkiwa wawili tu na jicho la Mungu ulidhani tamaa inapimwa kwa smartphone? Ulipoomuona kuwa yule jamaa ni mtanashati ukaamini kuwa hata nia yake ni tanashati ulikuwa hujui kuna samaki wenye mwiba mmoja uliojificha ndani ya mnofu na sasa umegundua kwakuwa mwiba umekukaba koo? Ulipokuwa unachukuwa zile pesa ili usitende haki kwakuwa ulikuwa unashida hukujua ni sio kila kipofu barabarani alikula rushwa na ukasahau kuwa rushwa huleta upofu? Ulipokubali kwenda na hujui ni wapi na kwanini ulidhani unaweza kupandisha mlimabila kuchoka? Ulipoamua kufanya kwa kuwa ulizidiwa nguvu na kwakuwa ulienda mwenyewe kwa kushawishiwa mnaenda kupiga tu story ulidhani ili iwe story ni lazima mvue nguo? Ulipoonywa na kukatazwa ulidhani wanakuonaea wivu kwa kiwango cha kujikataaa nafsi zao? Angalia ulipo sasa.


Ulishawishiwa. Ukaamini. Ukakubali. Ukaenda. Ukafanya. Ukaumia. Ukajuta. Ukasahau. Ukanogewa. Ukaendelea. Ukajisahau. Ukafika mwisho. Wenye dhambi wanapokushawishi huwezi kukataa kama huna sababu. Unaposhawishiwa kufanya uovu huwezi kukataa kama hauna wema wa kutosha ndani yako. Utakataaje na hujui kukubali. Kila jambo baya linapokuja kwako, uwezo wa kulikataa unategemea sana kiwango cha wema ulichonacho ndani maana katika hali ya kawaida huwezi kukataa jambo baya na hasa unalolipenda na linakuvutia kama uzuri unaoonekanakatika ubaya una nguvu. Kila mtu anashawishiwa lakini si kila mtu anashindwa na vishawishi. Fahamu kuwa ushawishi wa wenye dhambi unanoga zaidi kama hao wenye dhambi ni watu wetu wa karibu ambao tunawaamini na wamepata kibali ndani yetu. Alikwambia nisindikize na huku anajua yeye ndo anakusindikiza wewe kwani yeye alishazoea ila anakosa kampani na wakati wewe upo. Alikwambia anakupenda na kumbe anataka kujiliwaza baada ya kuachwa na kutendwa huko kwingine alikokuwa katika majaribio aliyoamua yanfanyikie mwili mwake. Jifunze kwanini Marekani huwa haipigani vita ndani ya ardhi yake, siku zote watawafuata adui zao huko wanakokaa.


NGUVU YA MAARIFA YA MUNGU
Njia ya pekee ya kijana kuweza kushinda mambo haya ni kuwa na maarifa ya kiMungu ndani yako na maarifa hayo chanzo chake ni KUMCHA BWANA kuishi katika hofu ya ukuu na utakatifu wake na kuendenenda chini ya mamlaka yake. Ni kuishi ukijua kuwa Mungu yupo na anatazamia uenende katika njia ikupasayo mbele zake. Maarifa ni ujuzi wa werevu au wa kujua, kuwa na maarifa ni kuwa na uwezo mkubwa wa kujua namna mbali mbali za kufanya jambo au mbinu amazo zote ni jumla ya ufahamu wako. Maarifa ni uwezo unaokuwa nao wa kujua namna gani utafanya ili uweze kuvuka. Ingawa maarifa yanahitaji hekima ili yawe na nguvu, yaani unaweza ukawa maarifa na hujui namna ya kuyatumia na hiyo ndiyo hekima. Na kumbe hekima ni kuwa na uwezo wa maarifa ya kujua au kufahamu kipi cha kufanya na ufanyaje, ufanye wapi na kwa muda gani. Chanzo cha maarifa ni kumcha Bwana. Utanaangamia kwa kukosa maarifa. Maarifa yako ndani ya Mungu na hakika ndani ya neno lake. Kama kumcha Bwana ndio chanzo cha maarifa, kumbe kiwango cha maarifa ya mtu kinategemea mahusiano yake na Mungu kwani kadri anavyokuwa karibu na Mungu ndivyo anavyopata maarifa ya kumsadia kushinda. Kama wewe kijana umeanguka katika nguvu ya ushawishi,ulitakiwa kukataa na ulishindwa kukataa kwakuwa hukuwa na maarifa maana hata kukataa sio lazima umtukane mtu ndo ajue umekataa. Kuna namna unaweza kusema HAPANA na unaemkatalia akajua hiyo ni bonge la NDIYO maana huna maarifa. Unaweza ukawa hujui namna ya kuishi na watu wasioamini unachoamini kwani huna maarifa ya kukusaidia kufanya hivyo.


Huwezi ukampenda Mungu halafu ukachukia maarifa yake, huwezi ukayapenda maarifa yake na ukamchukia Mungu maana yeye ndiye chanzo cha maarifa na ukiwa na Mungu basi unayo maarifa. Sio wote wanaosikia huelewa na wala sio wote wanaoelewa hufanya kama walivyoelewa na wala sio wote wanaofanya kama walivyoelewa hupatia kwani huenda alivyoelewa hakuelewa. Nakushauri leo chagua kumcha Bwana ili utembee katika maarifa ya Mungu katika maisha yako kama kijana na itakusaidia. Chagua kumcha Bwana kama unahitaji usalama na utulivu wa maisha yako yote hapa duniani na kutoka katika msongo wa mawazo. Amua kubadilika leo. Kusudia kubadilika leo na ubadilike. Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe Usikubali na hakika ukitembea na wapumbavu ni lazima utakuwa mpumbavu. Kagua watu wanaokuzunguka. Fanya tathmini nzuri na ukumbuke hayo ni maisha yako, sio ya kuazima na wala huwezi kumpa mtu mwingine akuishie kwa niaba na wala hakuna anaeweza kuwa wewe.

Jesus Up! YKM 2017
Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428