Mungu kwanza

Saturday, 4 August 2018

UBAYA HAUONEKANI KWA KUJIANGALIA KWENYE KIOO


Ni mtu aliyekusaidia sana katika kukua kwako na katika jitihada zako za kumtafuta Mungu. Anaweza akawa hakukusomesha wala kukulisha. Anaweza akawa hajakuzaa wala kukuvisha. Anaweza akawa hajakufahamu toka umezaliwa. Ila kuna namna toka mlipofahamiana amekusaidia sana na wewe unajua moyoni mwako. Inawezekana hajakaa na wewe miaka kumi, inawezekana ni nusu saa tu au siku nzima. Anaweza akawa hafanani na wewe kwa lolote. Lakini kuna vitu alijinyima kwa ajili yako.

Alitoa muda wake kukusikiliza ulipohitaji tu wa kukusikiliza. Alitoa nguvu yake ya mwili kuhakikisha hachoki kuendelea kukusikiliza. Kama alitoa muda wake basi alitoa na pesa zake ambazo hukuziona kwa macho ya kawaida. Wakati huo ulikuwa unamuelewa sana, ulikuwa unatamani awasiliane na wewe kila mara, ulitafuta hekima zake ambazo wakati huo zilikuwa kwako kama sega la asali. Wakati huo ulimtetea maana uliiona thamani yake. Wakati huo ulikuwa uko tayari kukosana na wasiomwelewa. Wakati huo ulihitaji mtu wa kuwa pamoja na wewe, ulimwita baba au mama au kaka au dada au mshauri au rafiki na kwakweli alikufaa sana.

Ulikuwa huoni haya kutambulishwa nae wala wewe kujiona uko chini ya malezi yake. Hata akiwa hayupo bado ulimsemea vizuri na hata katika mapungufu yake ulijua namna ya kumweleza ili asimame imara maana kuanguka kwake kutakuumiza. Hukutaka hilo litokee. Siku zikaenda. Ukakua. Ukapata ufahamu. Ukajiona uko huru. Ukapata elimu. Ukakutana na elimu kadhaa. Ukafundishwa mambo kadhaa. Moyo wako ukaanza kuona kumbe hata wewe unaweza. Hata wewe unajua. Hata wewe ni mtu. Kimsingi haujawahi kutokuwa hayo yote huko nyuma ila tu sasa unaona ni sawa zaidi.

Ukaanza kumuona anakuboa sana. Anakufuatilia sana. Tena kuna vitu wewe unavijua kuliko yeye. Kuna vitu Mungu anakuonyesha na vingine ni udhaifu wake na wewe kwako ukaona basi umeshakuwa juu yake. Thamani yake ikaanza kuporomoka ndani yako. Ule uchaji ukaanza kupauka. Ule upendo ukaanza kufifia. Ukaacha kumuita baba. Ukaacha kumuita mshauri. Ukaacha kumchukulia kama ni mtu sahihi tena kwako. Ukambadilishia jina lake. Ukaanza kuyaona mafundisho yake ni ya shetani. Ukaanza kujadili na kudhani kuwa wewe umesimama sana na Mungu. Ukasahau yote.

Kama sio wewe umefanyiwa hivi basi huenda wewe umemfanyia mwingine. Kama hujamfanyia basi chunga usije kufanya. Kama umefanyiwa samehe na achilia maana kisasi ni juu ya Bwana. Adui akiwa rafiki yako unaemwamini na kumpa fursa ya kukujua kuliko adui yako wa nje basi ujue huyu ni adui kweli kweli. Jifunze kuwa heshima ya mtu na utu wake, kama alikusaidia itabaki pale pale. Elisha alimhitaji Elia. Timothy na Paul. Daud na Sauli. Esther na Modecai. Musa na Yethro.  Paul na Barnabas. Wapo akina Ruth kwa Naomi.

Hata usipomwita baba au mama au kaka au dada. Safari haiishii kutokumuita. Ni mahusiano. Kuna leo na kesho pia. Acha majira na nyakati yawasukume mbali. Usimsukume mbali nawe. Ila bado maisha ni maamuzi. Mtu kama huyo basi hata muombee maana angeweza kufanya kwa wengine, akafanya kwako. Angeweza kuwa karibu na wengine lakini ukawa wewe. Wambali na wakaribu wote wana sehemu katika maisha yetu. Marafiki na maadui wote wana sehemu katika sisi kufikia hatma ya kutimiza kusudi la Mungu.

Yesu akawauliza…WATU WANASEMA YA KUWA MIMI NI NANI?


NAKUTAKIA BARAKA NA AMANI.


By Raphael JL: 0767033300
Classified Mindset 2018!
www.fichuka.blogspot.com
Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428