Mungu kwanza

Tuesday, 1 March 2022

NJE YA PENDO NI UTUMWA.(Upendo wa Mungu: Msingi wa Uhuru na Furaha Katika Ukristo)

Mateka anatakiwa kuhubiriwa kuhusu uhuru wake, sio tena jinsi alivyotekwa. Mfungwa anatakiwa kuhubiriwa kuhusu kufunguliwa kwake, sio habari ya kufungwa kwake. Na hii ndiyo habari njema, yaani Injili. Watu wanakuja kwa Yesu na mizigo yao ili wapate pumziko, sio kuongeza mzigo zaidi.

Ukristo sio sehemu ya kujikaza, wala sio eneo gumu. Mtu anatakiwa kufurahia kuwa Mkristo na kupata pumziko, sio tena uchovu. Tusiwafunge watu kwenye kongwa ambalo hata Waisraeli wenyewe hawakuweza kulibeba. Nira ya Kristo ni laini. Yeye ni Bwana wa Sabato (pumziko)【Mathayo 11:28-30】. 
Tumejiwekea mikakati mingi ya kumfikia Mungu jambo ambalo linawafanya wengine kuogopa kuwa Wakristo. Watu wanajikaza, wanaigiza, hawako halisi. Ukristo umekuwa sio pumziko tena.

Oh, kuna kitu kimeharibika mahali fulani. Tumejiwekea taratibu nyingi, mikakati mingi ya kumfikia Mungu. Tunachokosa ni upendo na maarifa. Ukiungwa na Mungu kwa upendo, huwezi kuhusiana naye kwa kanuni wala kwa msimu; inakuja kiotomatiki. 

1Yohana 4:7-8 inatukumbusha, "Wapenzi, na tupendane, kwa maana pendo latoka kwa Mungu. Na kila ampendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni pendo." Inafika mahali tunalazimishana kufunga, kuamka usiku kuomba, kusoma Neno, kutoa sadaka, nk. Mbona ukipenda hivi vitu vinakuja vyenyewe tena haviwi vya msimu fulani wala vya kanuni wala kulazimishana?

Imefika mahali tunawaalika wahubiri wengine ili wawafundishe waumini wetu kutoa. Maana unaona kama vile wewe ukiongea hawakuelewi. Akihubiri kwa wiki tatu za mwanzo, kiwango cha matoleo kinaongezeka. (Watu wanatoa kwa woga). Miezi sita mbele wanarudi kwenye hali yao ya awali. Shida iko wapi? Shida ni kwamba hawajafundishwa kwa kina kuhusu upendo wa Baba. Na kwao kutoa imekuwa utumwa, sio tena kitu wanachofurahia. 

2 Wakorintho 9:7 inasema, "Kila mtu na atoe kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni wala kwa lazima, maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."

Siku wakielewa upendo watafanya zaidi ya wafanyavyo sasa. Hawatajikaza kumtolea Mungu, watafurahia kumtolea. Hawatajikaza kufunga, watafurahia kufunga, hawatajikaza kuomba, watafurahia kuomba. 

Warumi 13:10  inatukumbusha, "Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria." Upendo utawabidisha. Shida ni kwamba watu hawajaelewa upendo wa Mungu kwao. Siku wakielewa, kutoa haitakuwa suala la kulazimishana, kuomba, kufunga nk haitakuwa suala la kulazimishana.

Upendo wa Mungu ulidhihirishwa kwa kumtoa Yesu【Yohana 3:16】. Hapa ndio kiini cha upendo. Tukielewa hapa, hayo mengine yatakuja kiotomatiki. 1 Yohana 4:19 inatukumbusha, "Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza."

Huwezi kupenda halafu ushindwe kujua namna ya kuhusiana na umpendaye. 1 Wakorintho 13:4-7 inaeleza, "Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote." Tungejawa na upendo, tusingekuwa na muda wa kuelekezana kuomba, kutoa, kusoma Neno, nk. Hatuna upendo, ndio maana tunapoteza muda kuelekezana na bahati mbaya haileti athari yoyote kwa sababu watu wanatoa kwa kulazimishwa, sio kwa upendo. Wanajikaza na mioyo yao haina furaha katika wanachofanya. Wanaigiza! Siku ukiacha kuwafundisha kutoa wenyewe wanaacha. Ukiacha kusisitiza maombi na wao wanaacha. Yaani utafikiri Mchungaji ndiye anayeharakisha kasi ya mchakato.

HUWEZI KUPENDA, UKASHINDWA KUTOA. KUTOA NJE YA UPENDO NI UTUMWA. KUFUNGA NJE YA UPENDO NI UTUMWA. Ukipenda sana na kuelewa upendo wa Mungu, utatoka kwenye kiwango cha "natoa ili nibarikiwe". Huu nao ni ubinafsi na kujihesabia haki. 
Warumi 5:8 inatukumbusha, "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi." Kwanini ulitoa nini kwa Mungu ili yeye amtoe Yesu kufa kwa ajili ya dhambi zako? Inafika mahali unategemea kiwango cha sadaka ulizotoa kuliko Mungu. Hivi Mungu angesema akubariki kwa kadiri ya matoleo yako, si ungekua ulishafilisika kitambo! Bwana anakubariki kwa kadiri ya utajiri wake, sio matoleo yako.Hata katika mahusiano ya kawaida ni hatari kuwa na mtu anayefanya kitu kwako ili wewe umfanyie kitu.


Uliyoyaelewa yachukue, ambayo bado hujaelewa yahifadhi, utayaelewa mbele.

Classified Mindsets
Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428