Mungu kwanza

Tuesday, 1 March 2022

NJE YA PENDO NI UTUMWA.(Upendo wa Mungu: Msingi wa Uhuru na Furaha Katika Ukristo)

Mateka anatakiwa kuhubiriwa kuhusu uhuru wake, sio tena jinsi alivyotekwa. Mfungwa anatakiwa kuhubiriwa kuhusu kufunguliwa kwake, sio habari ya kufungwa kwake. Na hii ndiyo habari njema, yaani Injili. Watu wanakuja kwa Yesu na mizigo yao ili wapate pumziko, sio kuongeza mzigo zaidi.

Ukristo sio sehemu ya kujikaza, wala sio eneo gumu. Mtu anatakiwa kufurahia kuwa Mkristo na kupata pumziko, sio tena uchovu. Tusiwafunge watu kwenye kongwa ambalo hata Waisraeli wenyewe hawakuweza kulibeba. Nira ya Kristo ni laini. Yeye ni Bwana wa Sabato (pumziko)【Mathayo 11:28-30】. 
Tumejiwekea mikakati mingi ya kumfikia Mungu jambo ambalo linawafanya wengine kuogopa kuwa Wakristo. Watu wanajikaza, wanaigiza, hawako halisi. Ukristo umekuwa sio pumziko tena.

Oh, kuna kitu kimeharibika mahali fulani. Tumejiwekea taratibu nyingi, mikakati mingi ya kumfikia Mungu. Tunachokosa ni upendo na maarifa. Ukiungwa na Mungu kwa upendo, huwezi kuhusiana naye kwa kanuni wala kwa msimu; inakuja kiotomatiki. 

1Yohana 4:7-8 inatukumbusha, "Wapenzi, na tupendane, kwa maana pendo latoka kwa Mungu. Na kila ampendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni pendo." Inafika mahali tunalazimishana kufunga, kuamka usiku kuomba, kusoma Neno, kutoa sadaka, nk. Mbona ukipenda hivi vitu vinakuja vyenyewe tena haviwi vya msimu fulani wala vya kanuni wala kulazimishana?

Imefika mahali tunawaalika wahubiri wengine ili wawafundishe waumini wetu kutoa. Maana unaona kama vile wewe ukiongea hawakuelewi. Akihubiri kwa wiki tatu za mwanzo, kiwango cha matoleo kinaongezeka. (Watu wanatoa kwa woga). Miezi sita mbele wanarudi kwenye hali yao ya awali. Shida iko wapi? Shida ni kwamba hawajafundishwa kwa kina kuhusu upendo wa Baba. Na kwao kutoa imekuwa utumwa, sio tena kitu wanachofurahia. 

2 Wakorintho 9:7 inasema, "Kila mtu na atoe kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni wala kwa lazima, maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."

Siku wakielewa upendo watafanya zaidi ya wafanyavyo sasa. Hawatajikaza kumtolea Mungu, watafurahia kumtolea. Hawatajikaza kufunga, watafurahia kufunga, hawatajikaza kuomba, watafurahia kuomba. 

Warumi 13:10  inatukumbusha, "Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria." Upendo utawabidisha. Shida ni kwamba watu hawajaelewa upendo wa Mungu kwao. Siku wakielewa, kutoa haitakuwa suala la kulazimishana, kuomba, kufunga nk haitakuwa suala la kulazimishana.

Upendo wa Mungu ulidhihirishwa kwa kumtoa Yesu【Yohana 3:16】. Hapa ndio kiini cha upendo. Tukielewa hapa, hayo mengine yatakuja kiotomatiki. 1 Yohana 4:19 inatukumbusha, "Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza."

Huwezi kupenda halafu ushindwe kujua namna ya kuhusiana na umpendaye. 1 Wakorintho 13:4-7 inaeleza, "Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote." Tungejawa na upendo, tusingekuwa na muda wa kuelekezana kuomba, kutoa, kusoma Neno, nk. Hatuna upendo, ndio maana tunapoteza muda kuelekezana na bahati mbaya haileti athari yoyote kwa sababu watu wanatoa kwa kulazimishwa, sio kwa upendo. Wanajikaza na mioyo yao haina furaha katika wanachofanya. Wanaigiza! Siku ukiacha kuwafundisha kutoa wenyewe wanaacha. Ukiacha kusisitiza maombi na wao wanaacha. Yaani utafikiri Mchungaji ndiye anayeharakisha kasi ya mchakato.

HUWEZI KUPENDA, UKASHINDWA KUTOA. KUTOA NJE YA UPENDO NI UTUMWA. KUFUNGA NJE YA UPENDO NI UTUMWA. Ukipenda sana na kuelewa upendo wa Mungu, utatoka kwenye kiwango cha "natoa ili nibarikiwe". Huu nao ni ubinafsi na kujihesabia haki. 
Warumi 5:8 inatukumbusha, "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi." Kwanini ulitoa nini kwa Mungu ili yeye amtoe Yesu kufa kwa ajili ya dhambi zako? Inafika mahali unategemea kiwango cha sadaka ulizotoa kuliko Mungu. Hivi Mungu angesema akubariki kwa kadiri ya matoleo yako, si ungekua ulishafilisika kitambo! Bwana anakubariki kwa kadiri ya utajiri wake, sio matoleo yako.Hata katika mahusiano ya kawaida ni hatari kuwa na mtu anayefanya kitu kwako ili wewe umfanyie kitu.


Uliyoyaelewa yachukue, ambayo bado hujaelewa yahifadhi, utayaelewa mbele.

Classified Mindsets
Share:

Sunday, 16 January 2022

TUMETOKA MBALI........!!



Kuna watu wana marafiki na wanasema wametoka mbali sana lakini cha ajabu hawajawapeleka mbali.....

Tangu rafiki yako awe fulani hata ibada umeacha,huwezi kuomba tena,umekuwa na tabia mbovu...

Tangu rafiki yako awe fulani huna heshima kwa mkeo na wala hujali kuhusu familia yako na huyo rafiki ameshauri uwe hata na kamchepuko...

Tangu rafiki yako awe fulani mmeo unaongea naye vyovyote vile bila adabu na wala hujali,
Tumekazana kusema this is my best friend since primary since childhood lakini hajakufanya uwe bora....

Rafiki yako ana mitazamo mibaya kuhusu ndoa, wanaume, wanawake hana interest na mafanikio unadhani utakuwa salama?
Rafiki yako anakuambia unaishije bila demu,unaishije kuwa tu mke lazima uwe na mchepuko je unadhani utakuwa salama??

Ni rafiki yako lakini huwezi kumwambia ukweli akikosea au akifanya kitu si sahihi eti kwamba unatunza urafiki unaogopa atakuchukia that's not friendship...

Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.
Mithali 13:20
Ukiwa na rafiki mpumbavu jiandae kuangamia,
Unaweza kuangamiza ndoa yako, biashara, huduma kisa marafiki ulionao.

Nani ni rafiki yako?
Tangu uwe naye mmesaidiana kuwa bora?
Umemzidi kumpenda na kumheshimu Mungu?? Jiulize kwa upole.

Choose wisely. 
Share:

Sunday, 2 January 2022

SALAMU ZA MWAKA MPYA WA 2022 TOKA KWA CHRISTOPHER NA DIANA MWAKASEGE


Bwana Yesu asifiwe sana katika mwaka huu mpya wa 2022; kuliko alivyosifiwa katika mwaka wa 2021. 
Je, uko tayari kwa kiwango gani, kuitikia wito wa Mungu, wa kutenda kazi pamoja naye, kwa njia ya maombi katika mwaka huu mpya wa 2022? 
Hili jambo ni kati ya mambo kadhaa, ambayo Mungu ametusisitiza tuyafanye kwa mwaka huu wa 2022. Nasi, tumeona, tukutumie wito  huu, kama salamu zetu za heri ya mwaka huu kwako, ili kukuhimiza uitikie wito huu! 
Si watu wengi, ambao wanaweza kutoa muda wao mwingi wa kuomba, ili kuombea mambo ambayo hayawahusu moja kwa moja. 
Watu walio wengi, wana utayari mkubwa, kutoa muda wao kuombea mambo yanayowahusu! Lakini kuna haja kubwa sana, mwaka huu, na miaka ijayo, kupata watu walio tayari, kutoa muda wao, kuombea mambo ambayo, wanaona hayawahusu moja kwa moja, lakini ni ya muhimu! 
Sijui kama unakumbuka ya kuwa: Maombi ni njia mojawapo, ambayo Mungu ameiweka, ili kuwapa wanadamu walio tayari, kufanya kazi pamoja naye, katika kulitimiza kusudu lake – hapa ulimwenguni. 
Je, uko tayari kutoa muda wako, kwa kiwango gani, mwaka huu tena kufanya kazi pamoja na Mungu kwa njia ya maombi? 
Hebu tizama na kutafakari mifano ifuatayo: 
Mfano wa 1: Mungu anatafuta “mtu” wa kuombea nchi, ili aturehemu na atusaidie (Ezekieli 22:30, 31 na 2 Mambo ya Nyakati 7:14). 
Mungu akimpata mtu wa kuombea nchi, mtu huyo atakuwa mmoja wa watendakazi pamoja na Mungu, katika nchi yao! Je, uko tayari kuitika? 
Mfano wa 2: Mungu anatafuta mtu wa kuombea miji, ili mipango ya miji hiyo isimame katika “ubunifu na misingi” ya Mungu (Waebrania 11:10); na wakazi wa miji hiyo, wapate msaada wa Mungu katika kufanikiwa kwao (Yeremia 29:7, 11 na Luka 19:41 – 44). 
Mungu akimpata mtu wa kuombea miji, mtu huyo atakuwa mtendakazi pamoja na Mungu, ndani ya huo mji. Je, uko tayari kuitika? 
Mfano wa 3: Tunaweza tusielewe ni kwa nini iwe hivi, lakini Mungu anapoona upungufu wa watendakazi wa kuchunga kondoo zake, huwa anatafuta mtu wa kuombea jambo hili (Mathayo 19:36 – 38). 
Je, uko tayari kuitika juu ya kuombea jambo hili mwaka huu? Ukikubali – utakuwa umeingia kuwa mmojawapo wa watendakazi pamoja na Mungu, katika kupata watendaji wake wa kuchunga kondoo zake (Luka 6:12 – 16). 
Mfano wa 4: Je, unafahamu ya kuwa, Mungu anataka apate mtu, wa kuomba kwa ajili ya watumishi, ili Mungu awalinde – utumishi wao usivurugwe au kuzuiwa? 
Soma Warumi 15:30 – 33; na Matendo ya Mitume 12:1 – 5; na Kutoka 17: 8 – 16. Je, uko tayari kuitika wito huu, wa kuombea watumishi wa Mungu, mwaka huu, kwa muda mwingi zaidi? 
Mfano wa 5: Je, unajua ya kuwa, ili Mungu athibitishe unabii ulio sahihi (Isaya 62:6, 7; na Luka 2: 36 – 38); na kupangua nabii zisizo sahihi (Matendo ya Mitume 16:16 – 18) – huwa anatafuta mtu wa kuombea nabii mbalimbali zinazotolewa na watu? 
Je, uko tayari kuitika wito huu, wa kufanya kazi na Mungu, kwa njia ya kuombea nabii mbalimbali, ili nabii zitolewazo, ziwe ni zile zilizo sawa na mapenzi ya Mungu, na zilizo sawa na neno lake? 
Mfano wa 6: Je, umeona kazi zo zote za Mungu “zilizokufa” katika mwaka 2021, na unataka kuona Mungu anazifufua upya, katika mwaka 2022? Basi, unahitaji kuwa mmoja wa watu wa kuombea jambo hili! Je uko tayari? Soma Habakuki 3:1, 2, 3. 
Mfano wa 7: Je, unataka kuona vijana – wa kiume na wa kike, wanakuwa na hali nzuri kiroho, na kimaisha, na kiakili, katika mwaka 2022, kuliko ilivyokuwa mwaka 2021? 
Unahitaji kuwa mmoja wa wale wanaowaombea vijana. Na Mungu atajibu maombi yako, na atawasaidia vijana hao (Yeremia 9:17 – 21). 
Mfano wa 8: Eneo mojawapo linalohitaji maombi, ili nchi iwe na “utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu” (1 Timotheo 2:1, 2); ni kuombea viongozi, na “wote wenye mamlaka”! 
Mungu anahitaji watu tena kwa mwaka 2022, watakaobeba mzigo wa kuombea “wote wenye mamlaka”; ili Mungu atumie maombi yao, kutulinda na kututunzia amani, ili nchi iwe na utulivu. Je, uko tayari kuitika wito huu?
Mfano wa 9: Ukiona limejitokeza jambo la mabishano juu ya Mungu yupi, ndiye mkubwa, na yupi afuatwe na watu – ujue eneo hilo linahitaji maombi ya 1 Wafalme 18:36 – 39. 
Je, uko tayari kuitika wito huu, wa kuomba maombi ya jinsi hii, kwa mwaka 2022? Ukiukubali wito huu, ujue utafanyika mtendakazi pamoja na Mungu, kwa njia ya maombi, kwenye eneo hili. 
Mfano wa 10: Je, kuna eneo lo lote ambalo hukuona mapenzi ya Mungu yakitimizwa, au kutekelezwa ipasavyo, katika mwaka 2021. Je, unataka kuona eneo hilo, likitimiza na kutekeleza mapenzi ya Mungu ipasavyo, katika mwaka huu wa 2022? 
Ikiwa majibu yako ni ndiyo, katika maswali haya mawili, ujue unahitaji kutenga muda wa kuombea eneo hilo, sawa na Mathayo 6:9, 10. Je, uko tayari kufanya maombi ya jinsi hii? 
Hii mifano michache, tuliyokupa katika salamu hizi, iwe kichocheo ndani ya moyo wako,ili utenge muda kwa mwaka 2022, kuombea mojawapo, au zaidi, ya mambo yaliyomo katika mifano hiyo. 
Tuzidi kuombeana. 


Usisahau kuungana nasi, kwenye semina ya kufungua mwaka wa 2022, tutakayoifanya Arusha mjini – uwanja wa Reli, tarehe 5 – 9 Januari. Tutairusha pia kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428