Mungu kwanza

Sunday, 2 January 2022

SALAMU ZA MWAKA MPYA WA 2022 TOKA KWA CHRISTOPHER NA DIANA MWAKASEGE


Bwana Yesu asifiwe sana katika mwaka huu mpya wa 2022; kuliko alivyosifiwa katika mwaka wa 2021. 
Je, uko tayari kwa kiwango gani, kuitikia wito wa Mungu, wa kutenda kazi pamoja naye, kwa njia ya maombi katika mwaka huu mpya wa 2022? 
Hili jambo ni kati ya mambo kadhaa, ambayo Mungu ametusisitiza tuyafanye kwa mwaka huu wa 2022. Nasi, tumeona, tukutumie wito  huu, kama salamu zetu za heri ya mwaka huu kwako, ili kukuhimiza uitikie wito huu! 
Si watu wengi, ambao wanaweza kutoa muda wao mwingi wa kuomba, ili kuombea mambo ambayo hayawahusu moja kwa moja. 
Watu walio wengi, wana utayari mkubwa, kutoa muda wao kuombea mambo yanayowahusu! Lakini kuna haja kubwa sana, mwaka huu, na miaka ijayo, kupata watu walio tayari, kutoa muda wao, kuombea mambo ambayo, wanaona hayawahusu moja kwa moja, lakini ni ya muhimu! 
Sijui kama unakumbuka ya kuwa: Maombi ni njia mojawapo, ambayo Mungu ameiweka, ili kuwapa wanadamu walio tayari, kufanya kazi pamoja naye, katika kulitimiza kusudu lake – hapa ulimwenguni. 
Je, uko tayari kutoa muda wako, kwa kiwango gani, mwaka huu tena kufanya kazi pamoja na Mungu kwa njia ya maombi? 
Hebu tizama na kutafakari mifano ifuatayo: 
Mfano wa 1: Mungu anatafuta “mtu” wa kuombea nchi, ili aturehemu na atusaidie (Ezekieli 22:30, 31 na 2 Mambo ya Nyakati 7:14). 
Mungu akimpata mtu wa kuombea nchi, mtu huyo atakuwa mmoja wa watendakazi pamoja na Mungu, katika nchi yao! Je, uko tayari kuitika? 
Mfano wa 2: Mungu anatafuta mtu wa kuombea miji, ili mipango ya miji hiyo isimame katika “ubunifu na misingi” ya Mungu (Waebrania 11:10); na wakazi wa miji hiyo, wapate msaada wa Mungu katika kufanikiwa kwao (Yeremia 29:7, 11 na Luka 19:41 – 44). 
Mungu akimpata mtu wa kuombea miji, mtu huyo atakuwa mtendakazi pamoja na Mungu, ndani ya huo mji. Je, uko tayari kuitika? 
Mfano wa 3: Tunaweza tusielewe ni kwa nini iwe hivi, lakini Mungu anapoona upungufu wa watendakazi wa kuchunga kondoo zake, huwa anatafuta mtu wa kuombea jambo hili (Mathayo 19:36 – 38). 
Je, uko tayari kuitika juu ya kuombea jambo hili mwaka huu? Ukikubali – utakuwa umeingia kuwa mmojawapo wa watendakazi pamoja na Mungu, katika kupata watendaji wake wa kuchunga kondoo zake (Luka 6:12 – 16). 
Mfano wa 4: Je, unafahamu ya kuwa, Mungu anataka apate mtu, wa kuomba kwa ajili ya watumishi, ili Mungu awalinde – utumishi wao usivurugwe au kuzuiwa? 
Soma Warumi 15:30 – 33; na Matendo ya Mitume 12:1 – 5; na Kutoka 17: 8 – 16. Je, uko tayari kuitika wito huu, wa kuombea watumishi wa Mungu, mwaka huu, kwa muda mwingi zaidi? 
Mfano wa 5: Je, unajua ya kuwa, ili Mungu athibitishe unabii ulio sahihi (Isaya 62:6, 7; na Luka 2: 36 – 38); na kupangua nabii zisizo sahihi (Matendo ya Mitume 16:16 – 18) – huwa anatafuta mtu wa kuombea nabii mbalimbali zinazotolewa na watu? 
Je, uko tayari kuitika wito huu, wa kufanya kazi na Mungu, kwa njia ya kuombea nabii mbalimbali, ili nabii zitolewazo, ziwe ni zile zilizo sawa na mapenzi ya Mungu, na zilizo sawa na neno lake? 
Mfano wa 6: Je, umeona kazi zo zote za Mungu “zilizokufa” katika mwaka 2021, na unataka kuona Mungu anazifufua upya, katika mwaka 2022? Basi, unahitaji kuwa mmoja wa watu wa kuombea jambo hili! Je uko tayari? Soma Habakuki 3:1, 2, 3. 
Mfano wa 7: Je, unataka kuona vijana – wa kiume na wa kike, wanakuwa na hali nzuri kiroho, na kimaisha, na kiakili, katika mwaka 2022, kuliko ilivyokuwa mwaka 2021? 
Unahitaji kuwa mmoja wa wale wanaowaombea vijana. Na Mungu atajibu maombi yako, na atawasaidia vijana hao (Yeremia 9:17 – 21). 
Mfano wa 8: Eneo mojawapo linalohitaji maombi, ili nchi iwe na “utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu” (1 Timotheo 2:1, 2); ni kuombea viongozi, na “wote wenye mamlaka”! 
Mungu anahitaji watu tena kwa mwaka 2022, watakaobeba mzigo wa kuombea “wote wenye mamlaka”; ili Mungu atumie maombi yao, kutulinda na kututunzia amani, ili nchi iwe na utulivu. Je, uko tayari kuitika wito huu?
Mfano wa 9: Ukiona limejitokeza jambo la mabishano juu ya Mungu yupi, ndiye mkubwa, na yupi afuatwe na watu – ujue eneo hilo linahitaji maombi ya 1 Wafalme 18:36 – 39. 
Je, uko tayari kuitika wito huu, wa kuomba maombi ya jinsi hii, kwa mwaka 2022? Ukiukubali wito huu, ujue utafanyika mtendakazi pamoja na Mungu, kwa njia ya maombi, kwenye eneo hili. 
Mfano wa 10: Je, kuna eneo lo lote ambalo hukuona mapenzi ya Mungu yakitimizwa, au kutekelezwa ipasavyo, katika mwaka 2021. Je, unataka kuona eneo hilo, likitimiza na kutekeleza mapenzi ya Mungu ipasavyo, katika mwaka huu wa 2022? 
Ikiwa majibu yako ni ndiyo, katika maswali haya mawili, ujue unahitaji kutenga muda wa kuombea eneo hilo, sawa na Mathayo 6:9, 10. Je, uko tayari kufanya maombi ya jinsi hii? 
Hii mifano michache, tuliyokupa katika salamu hizi, iwe kichocheo ndani ya moyo wako,ili utenge muda kwa mwaka 2022, kuombea mojawapo, au zaidi, ya mambo yaliyomo katika mifano hiyo. 
Tuzidi kuombeana. 


Usisahau kuungana nasi, kwenye semina ya kufungua mwaka wa 2022, tutakayoifanya Arusha mjini – uwanja wa Reli, tarehe 5 – 9 Januari. Tutairusha pia kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428