Jesus Up!
Ulishasikia watu wakisema mtu ana nidhamu ya woga? Au wewe mwenyewe ulishawahi kumuheshimu mtu kwa kumuogopa? Yaani unamuogopa mpaka unamuheshimu kwa kiwango ambacho unakuwa mtumwa anaetumikishwa na upumbavu wake mwenyewe akijua ni mtoto mtiifu. Ngoja nikuelezee vizuri.
Kuna utofauti mkubwa sana kati ya kuwa muoga na kuwa na heshima, hivi vitu viwili vina ukaribu sana na ni rahisi sana kuvichanganya na hasa kama uko upande unaoonewa zaidi. Niseme, kumuogopa mtu sio kumuheshimu na wala kumuheshimu sio kumuogopa ila inawezekana kabisa ukawa unanidhamu ya woga inayokufanya wewe ulazimike tu hata kuheshimu kwani huna namna nyingine ya kufanya. Nidhamu ya woga ni moja kati ya utumwa wa kijinga ambao unaweza ukawa juu ya mtu kwa mtu mwingine. Ninalozungumza ni jambo la kimahusiano na sio nadharia ya uandishi. Kama ulishawahi kumheshimu mtu kwa kumuogopa utaelewa ninachosema. Nitajitahidi kutoa mifano halisi kwa kadri nitakavyoweza ili kuhakikisha kuwa unapata dhima ya ujumbe huu na utaelewa kwanini nimesema nidhamu ya woga iiliyomfanya muoga kudhani ana heshima na kumbe ni uoga wake tu. Na kwa upande wa pili yuke anaeheshimiwa kwa uoga wa namba hii anaweza akadhani anaheshimiwa kweli kweli kwasababu ya vipaji na vipawa alivyonavyo na kumbe watu wana muogopa.
Kama wewe ndo unaegopwa unaweza usipende sana kusoma ujumbe huu wote lakini nakusihi usome tu maana yale yanayotuuma na tunayoogopa kuyasikia ndio ufunguo wa vifungo vingi sana kwetu. Na kama wewe ndio unaeogopa ukidhani unaheshima utashangaa kujua kuwa hujawahi kuwa na heshima ila umejaa unyenyekevu wa mtoto wa kambo anaelishwa chakula cha hasira na mama wa kambo.
Natamani ujue kuwa, ni kweli kuwa unaweza kumuheshimu mtu kwakuwa unamuogopa ingawa inatakiwa umuheshimu mtu kwasababu ya utu kwanza, yaani kwakuwa wewe ni binadamu na yeye pia basi kila mtu anastahili heshima. Ujumbe wangu wa leo unataka kuzungumzia eneo moja tu lenye watu wawili ambao wote ni wahanga wa jambo hili, kama mimi. Wote wawili wana sifa na tabia zinazowafanya waishi kati upande mmoja wa sarafu. Tutachunguza tuweze kuona kwa kina.
Kumuheshimu mtu kwa nidhamu ya woga ni kumharibu na kujiharibu, kimsingi ni moja kati ya viwango vya juu sana vya unafiki wa pande zote mbili. Yaani kwa upande wa anaeogopwa akidhani anaheshimiwa na akaridhika inakuwa ni ishara kiburi na majivuno na ubinafsi kwa ujumla wake. Na anaeogopa akidhani anaheshima basi unakuwa ni uoga wa kumfanya atumikie hata mambo asiyoyapenda ilimradi tu aonekane ana heshima. Anakuogopa kama hawezi kukwambia ukweli na hasa kwenye maeneo unayohitaji msaada, yaani mapungufu yako. Okay, kwahiyo mimi kushauriwa na kushaurika na mtu ninayemuongoza na niliyemzidi kila kitu isipokuwa tu kwamba wote bado tunapumua ni ishara ya kuelewa umuhimu wa heshima. Yaani, kama mtu mdogo ambaye labda unamuita mtoto wa kiroho au wewe kwake ni mfano au mwalimu au Mchungaji au mbunge akawa hana uwezo wa kukwambia ukweli pale unapokosea au kukwambia udhaifu wako ili ubadilike ni ishara kwamba ana nidhamu ya woga.
Mtu unaemwambia kila kitu nay eye kwake jibu ni ndio tu kwa kila kitu hata kama ni hatarishi kwenu nyote na hawezi kutoa hata maelezo yoyote ya msingi ya kukubali, hii ni dalili ingine kwamba nidhamu ya woga ipo kwenye viwango vyake vya utekelezaji. Mtu anaekutetea kwa watu wengine ambao hawajui vizuri ya kwamba wanakujua wewe kuliko yeye maana yeye ni mpenzi au mfuasi lakini yuko tayari kukutetea kwa kiwango cha kumaanisha kuwa wewe huwezi kukosea na wala hujawahi kukosea na ukikosea basi kosa ndo lina kosa na sio wewe. Unadhani hapa kuna heshima kwa kiwango gani?
Unapotoa kazi za kufanya, mtu anajua kabisa uwezo wake lakini bado atakomaa tu na kubeba mzingo asioweza kuufanya ili mradi tu usimuelewe vibaya na ili asikuumize na mwisho anakuumiza zaidi kwa kufanya chini ya kiwango. Hapa naomba tuelwe kuwa mashabiki wengi ni watu wa ajabu sana. Anaweza kukushabikia hata ujinga wako maana ndo unaitwa upendo wa kweli. anasahau kuwa heshima inajengwa na utu kabla ya upendo. Yaani hata kama humpendi, ana haki ya kuheshimiwa kama binadamu.
Umesikia madhaifu ya mtu unaemwamini sana, yaani unaamini siwezi kukosea, unajua najua mengi sana yaani kama vile mimi ni kamusi inayotembea, najua kila kitu, nina ushauri kila sekunde na tena ushauri wa kila aina. Unapiga mahesabu ya utamwambiaje udhaifu wake mtu kama huyo. Na ten ahata hutaki kukubali kama mtu kama huyo unaemuita baba sijui dad siju mentro au mwalimu au vyovyote vile anaweza kuwa kwenye kiwango kama hicho cha udhaifu. Labda hujawahi kumuona akilia, hujawahi kumuona akifuta machozi, hujawahi kumuona akiumia, hujawahi kusikia akisema na yeye ana changamoto kama zako ila viwango tu viko tofauti.
Unaogopaje kumsaidia mtu unaempenda? Mtu unaemwamini kuliko unavyojiamini? Kwanini usikatae kufanya kama unajua huwezi? Kwanini kulazimisha mambo ili machoni uonekane uko sawa lakini moyoni unajuta? Kwanini usiwe mkweli angalau mara moja tu? Kwanini ukae kimya na kinakuuma kwamba hakuelewi? Upo mtego.
Upo mtego, kumbuka mtego hutegwa kwa ndege yoyote yule. Vijana wengi wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kufanya mambo huwa ni vigumu sana kuwashauri na huwa hawashauriki kirahisi na mara nyingi huleta magomvi mengi tu. Vijana wengi wameanzisha vitu vikubwa na wengine kuliko miili yao au majina yao au elimu zao au wakubwa zao na hawa ili umshauri kama humuogopi unakuwa umefika kwenye hatua ambayo uoendo una nguvu sana . jipime, watu wanaokuzunguka na hasa wale uliowazidi mambo mengi wana uwezo gani wa kukuonya?
Wanaweza kweli wakanionya mimi YKM Founder? Wakanambia mapungufu yangu kweupee? Wakanambia jinsi ninavyopenda sifa tena za kijinga? Wanaweza wakanambia kuwa nilikosea? Wanaweza. Kabisa upande huo wapo wanaoniheshimu pasipo hofu na wanaweza kunambia lolote. Sitasahau nilipokaa na viongozi wangu wa YKM taifa na wakaanza kunizodoa na kunambia mapungufu yangu, ilikuwa inauma lakini inaingia. Yaani watu ninaowaongoza, wengine nimewatoa jalalani huko, wengine hata walikuwa hawajijui wakiwa katika ujinga wa ujanja wao, leo wananambia baba pale ulichemka na kuna namna wewe sio mnyenyekevu kabisa. Kwamba napenda sifa na nina kiburi. Inauma sana. Lakini wao wanakuwa wametimiza wajibu wao mkuu kwangu. Wajibu wa kunifundisha ili chuma kinoe chuma.
Mtego ni kama mimi niko tayari kuwasikia, niko tayari kuwaelewa na kubadilika ili mahusiano yetu yaendelee kuboreka kila iitwapo leo. Kama nitabaki na nafasi yangu, mimi ndo Founder, mimi ndio dad sijui, mimi ndo nabii je hawa watu nitafanya nao kazi vizuri?
Lazima kila mmoja wetu apambanue, ni bora usiheshimiwe kuliko nidhamu ya woga maana inakusaidia kupotea na inakufanya uwe na imani na nyumba ya biskuti wakati wa masika. Inauma sana kuambiwa ukweli na watu wa karibu na hawa wale walio chini yako lakini hao ndo wanakufaha na wanaweza kukuelezea vizuri zaidi maana wameona unavyofanya na kuishi kila siku. Ni bora kukaa peke yako, kuliko kuwaleta watu karibu ukidhani wamekuja kusheza shoo, watakukagua kila unalofanya na wale wanaokupenda na kukuheshimu kwa dhati hawatakaa kimya bali watasema kilaunapoleta mambo yako ya ubabe. Usiwachukie, wapende na uwashukuru maana wako hapo kwa niaba yako. Usiwatenge, wakubali maana hakuna mtu duniani aliyewezakufanya mambo makubwa peke yake. Yaani tunahitajiana katika kutokukamilika kwetu na kwakuwa wote hatujakamilika basi uikamilifu wetu uko kwa wengine.
Moja na moja ni mbili, hapo pana siri kubwa sana. Wito wangu kwa vijana wote walio na maono makubwa na walio na huduma kubwa au biashara kubwa ni muhimu kujua ni aina gani ya watu unaowatengeneza karibu yako. Je, unataka watu walioficha heshima ndani ya woga au kinyume chake. Kwa vyovyote vile, ni vizuri watu wanaotuzunguka wakatuamini kwa kiwango ambacho hata wakiwa mbali na sisi bado wanaweza kuelezea uzuri na ubaya wetu bila majungu au fitini ndani yake. Nimeona nidhamu za woga zinavyoleta matumaini ya muda mfupi na kwa hakika unaweza kumuacha mtu anaekupenda kwa kukwambia ukweli na ukaambatana na mtu anaeigiza heshima kwani mazingira yanaruhusu. Wengi sana hutafuta kibali kwa njia hii, yaani kwa njia ya uigizaji na unafiki, unaweza mpaka ukashawishika kuwa anakuheshimu lakini kimsingi anakuogopa kuliko anavyoogopa dhambi.