Mungu kwanza

Saturday, 30 December 2017

VUMBUA KAZI YA MUNGU NDANI YAKO


VUMBUA KAZI YA MUNGU NDANI YAKO MWAKA 2015
FANIKIWA JUU NA NJE YA MIPAKA YA MAISHA ULIYOZOEA
Mwaka 2014 umeisha. Majira yake yamepita. Kwa wengi imebaki kumbukumbu ya furaha na au maumivu ya mambo yaliyotokea mwaka 2014. Leo ni siku mpya, siku mpya inayoanzisha upya wa mwaka mzima wa 2015. Lazima yapo ya kujifunza kwa mwaka 2014. Yapo ya kuyabeba na kuingia nayo mwaka 2015. Wapo watu wa kuwaacha au kukaa nao mbali mwaka 2015 hata kama walikusaidia mwaka 2014. Majira yana nguvu kuliko wewe. Usipoyatii hayaumii. Usipoyazingatia utajiumiza wewe na kuwaumiza wanaokuzunguka. Historia imekamilika leo. Historia ya mwaka 2014. Watu na mambo yaliyotokea, magumu na mepesi. Maeneo uloenda na mambo uloyafanya. Hiyo ni historia. Matukio na majira na nyakati. Mahali na watu. Historia imekamilika. 2014 umepita. Kuishi kwa yaliyopita na hasa kama ni mabaya ni maamuzi.

NGUVU YA KUTAFSIRI MAMBO
Leo ni siku ya kwanza kati ya siku 365, zinazotengeneza mwaka mzima wenye miezi kumi na mbili. Mwaka mpya 2015. Leo ni siku ya kwanza ya upya wa mwaka mpya wa 2015. Leo ni siku ya kwanza ya upya wa mwezi wa kwanza. Mwaka huu ni mpya kwani haujawahi kuonekana na watu wala kutumika. Hakika ni mwaka mpya kwa kila sababu. Kwa mwaka huu mpya wewe ni yule yule lakini unatakiwa kuishi katika upya wa mwaka huu. Ni muhimu sana, katika mwanzo wa mwaka huu na mwezi huu kutafsiri kwa usahihi mambo yote yaliyo mbele yako ikiwa ni pamoja na kuutafsiri mwaka huu kwa upana wake. Ili uweze kutafsiri vizuri mambo yote ni lazima uwe na ufahamu na uelewa mzuri wa kukusaidia kuyaelewa mambo. Hapa, mambo ya kutafsiri namaanisha;
Mambo unayoona
Mambo unayosikia
Namna unavyoelewa
Nguvu ya kutafakari
Mwaka huu ni mpya. Nini si kipya ndani yake? Mhubiri 3:1-10. Mungu yuko juu ya majira. Mungu yuko juu ya nyakati. Mungu anamiliki majira na nyakati na ni yeye aliyeziweka. Mwaka 2015 ni majira. Majira mapya kwetu lakini kwa Mungu ni si jambo jipya. Kwamba umeuona mwaka huu mpya wa 2015 ujue Mungu alishakamilisha kila kitu kwa ajili yako. Mungu anaujua mwaka wote wa 2015. Anajua nini kitatokea mwezi wa kumi 2015. Anajua hazina alokuwekea ili ufanikiwe mwaka huu. Anaujua mwisho wa mwaka huu na ndio maana ameuruhusu uwepo na mimi na wewe tuuone. Kwamba tumeuona ni ushahidi kwamba lipo kusudi. Anayelijua kusudi ni aliyeweka mwaka na wala sie anaishi ndani yake. Efeso 2:10. Usikosee kuelewa. Usikosee kupanga.
Yapo mambo mema ambayo Mungu alikwisha kuyaanzisha ili wewe uyafanye na ukiyafanya basi ufanikiwe. Kumbuka, mafanikio yako kwa mwaka huu 2015 yanategemea sana uwezo wako wa kuvumbua kazi ya Mungu ndani yako na wengine na kuifanyia kazi. Kuvumbua. Discover. Huwezi ukayafanya mema usiyoyajua. Vumbua uwezo ulio ndani yako. Uvumbuzi huwa unamfanya mvumbuzi kuishi nje na Zaidi ya mipaka. Ndio, mipaka. Mipaka ya mazingira. Mipaka ya elimu. Mipaka ya ufahamu. Mipaka ya udini. Mipaka ya udhehebu. Mipaka ya utaifa. Mipaka ya aina ya watu. Wavumbuzi wengi walivunja mipaka yao ya ukabila baada ya kuvumbua uwezo waliokuwa nao ndani. Kuvumbua ni kazi nzito kidog… Read more
00:05
 30. 03. 2015
UDANGANYIFU WA MOYO: ALIYE KARIBU NA WEWE ANA NAFASI KUBWA ZAIDI YA KUKUSHAIWISHI.
Jesus Up!
Yeremia 17:9,10 moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.
Ni ukweli usiopingika kwamba moyo una udxanganyifu wa ajabu sana na kwa bahati nzuri wa kimkakati ni Mungu tu ndiye anaeufahamu moyo wa kila mtu. Nia ya mtu ndio inayomtengenezea sababu kuu ya kufanya chochote anachofanya na swali la kugundua nia mar azote limekuwa KWANINI. Kwanini unanipenda, kwanini mimi? Kwanini. Kwanini. Kwanini.

Leo nataka niongelee udanganyifu wa  moyo kwa upande wa mahusiano na hasa hicho kipande cha aliye karibu na wewe ana nafasi kubwa zaidi ya kukushawishi kukosea au kupatia. Aliye karibu na wewe hakujikuta karibu na wala wewe hukujikuta karibu yake. Kama mlifanikiwa KUJIKUTA basi ndo maana usome mpaka mwisho maana hilo neno NIMEJIKUTA limewakosesha wengi na kuwafanya wasiwajibike katika maisha yao. Mahusiano huanzia mbali kwanza. Kumbuka hujazaliwa tumbo moja nae bali umekutana nae shule. Umekutana nae kanisani. Umekutana nae madrasa. Umekutana nae kwenye kigango wakati wa novena. Umekutana nae njia au barabarani. Kwanza mlikuwa hamuwezi hata kusalimiana. Mlikutana nae kwenye gari mkakaa siti moja. Mlikutana facebook. Kila uhusiano wa kimapenzi kuna mahali ulianzia. Sio tu kuwa kuna mahali ulianzia bali cha muhimu kingine ipo sababu iliyoanzisha mahusiano hayo ambayo huenda yalionekana ni ya kawaida mwanzoni lakini yakakua. Sio tu sababu ya kuanzisha mahusiano hayo bali pia namna yalivyoanza bila kusahau muda na hali uliyokuwa nayo wakati urafiki unaanza.
1. Kila mahusiano kuna mahali yalianzia
2. Kila mahusiano yalianza kwa sababu fulani
3. Kila mahusiano yalianza kwa namna fulani
4. Kila mahusiano yalianza kwa muda wa wakati fulani
5. Hali uliyokuwa nayo wakati unaanza kutengeneza mazingira ya mahusiano yoyote ni muhumu kama maisha yako yenyewe

Kumbuka ukaribu ni matokeo ya uwekezaji na uwekezaji ni mkakati wenye kukupa mwelekeo wa kufikia kule uendako, jiulize unawekezaje?. Yapo ya kujiuliza hapa, kwanini amekuwa karibu yeye na sio mwingine, amekuwa karibu na wewe bila wewe kujua, umejikuta tu, Bwana alikuonyesha au uliota ndoto? Hata kama Bwana alikuonyesha bado unakazi kubwa ya kujenga ukaribu ili uyafaidi mahusiano. Hata kama ulimuota ndotoni bado kujenga ukaribu ni jukumu zito kwako ili uweze kufaidi na pia ni vizuri kufahamu kuwa kuna mambo au kuna kina cha uhusiano hutaweza kufika mpaka umejenga ukaribu na nakukumbusha kuwa aliye karibu na wewe anao uwezo mkubwa sana wa kukushawishi kufanya au kutokufanya, kwenda au kutokwenda. Ukaribu ni msingi wa mahusiano yoyote na kinyume chake pia. Nitaelezea vizuri hayo mambo matano na mengineyo hapo mbele kidogo ila kwa leo niweke huu msingi vizuri kuwa kuna uhusiano wa nani anaekusaidia kukosea au kupatia kutegemea ukaribu wake kwako na ukaribu wako kwake. Ndani ya huu ukaribu au umbali ndipo kuna kipande cha kwanza cha ujumbe huu yaani UDANGANYIFU WA MOYO. Yaani katika ukaribu wa aliyekaribu yako ndani yake kuna vitu vinaweza kuwa ni udanganyifu wa moyo na pasipo kujua ukatumbukia katika uharibifu ambao hutaweza kutoka mpaka kwa nguvu ya ziada. Yaani kuna watu umewaruhusu kuwa karibu na wewe na wengine unawakwepa kabisa. Inawezekana kuwa zipo sababu nzuri kabisa za kwanini wako karibu na kwanini wengine wako mbali na hata hivyo hawawezi wote wakawa karibu na mbali kwa wakati mmoja.

Maana ya udanganyifu wa moyo: Maana yake nia iliyoharibika, maana yake kufanya kitu ukiwa na sababu ya uongo au isiyo ya kweli au kufanya kwa hila au kuutumia unafiki kama njia ya kupata unachotaka au kuficha uhalisia wa jambo na kuleta kinyume chake ili kunufaika kwa jambo. Maana yake katika kufanya jambo mtu anakuwa na uharibifu wa nia yake na kusimamia msingi wa sababu isiyofaaa kwake na kwa mwininge ingawa kwa wakati wa mwanzo kwa upande wake anaweza kufurahia. Wrong motive. Wrong and bad intentions cant produce a right results. Moyo wa mtu unaweza kudanganywa na kumbadilisha maamuzi na nia yake kwa vitu kadhaa, mfano Mithali 31:30, upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili…

Maana ya ukaribu: Ni vigumu kuelezea maana ya ukaribu kuliko kuwa katika ukaribu, yaani ukaribu unaweza ukaelezewa kwa uzuri zaidi kwa vitendo. Najua una watu wako karibu na wengine wako mbali nawe. Hiyo ndiyo maana ya ukaribu.
Tutaangalia kwa kina namna moyo uliodanganywa unavyoweza kuwa msingi wa kukosea katika maamuzi kwa kupima ukaribu tulio nao na watu kadhaa katika maisha yetu.

Nitaendelea.
YKM Founder.




31.03.2015
UDANGANYIFU WA MOYO: ALIYE KARIBU NA WEWE ANA NAFASI KUBWA YA KUKUSHAWISHI-MLIKUTANIA WAPI INA NGUVU SANA
Jesus Up!
Nilisema na nataka kukazia kuwa watu wa karibu yetu ndio wenye nguvu kubwa ya kutushawishi kupatia ama kukosea katika maamuzi yetu ambayo ndio maisha yetu kimsingi. Ukaribu sio tu kutembea pamoja au kuwa mahali pamoja na huyo mtu au hao watu bali ni ile ruhusa inayompa mtu kibali ndani ya moyo wake au kinyume chake. Yaani, mtu anaweza akawa Sumbawanga na mwingine yuko Urusi lakini bado wakawa karibu sana. Kumbuka hili jambo linahusu mahusiano. Katika hili ndo nikasema inawezekana kukawa na udanganyifu ndani yake. Leo nataka kupiga hatua moja mbele na kimsingi nataka nizungumzie mojawapo yay ale mambo yetu matano tuliyoangalia kwenye sehemu ya kwanza. Kumbuka nilisema ukaribu ni matokeo, yaani ukaribu hutengenezwa, yaani ukaribu ni hatua endelevu na ya kwamba ukaribu unajengwa na pia unaweza kubomolewa. Uwezekano mkubwa ni kuwa mambo yale yale yanayojenga yanaweza pia kubomoa ukaribu na tufahamu kuwa ukaribu ukiharibiwa na kubomolewa basi umbali huzaliwa na umbali ukizaliwa maana yake nguvu ya ushaiwishi juu ya huyo mtu inapungua na mwisho kuondoka kabisa.
Ukaribu huanzia mahali fulani, yaani kila mahusiano kuna mahali yalianzia, location. Mlikutania wapi na huyo mtu uliyekaribu nae ina nguvu sana kama nguvu ya mahusiano yenyewe. Mlikutania wapi. Mlianzia wapi kujenga ukaribu maana ukaribu una mwanzo na huo mwanzo ni lazima ulitokea mahali fulani. Yaani ni lazima. Mfano, ulikutana nae disco, okay mkakaa pamoja, siku akikwambia aende disco kidogo utashangaa? Mahali mlipokutania pana maana kubwa sana kwani huwa panatumika kama madhabahu ya kuwaunganisha watu na pia kuwatengenisha. Fikiria umekutana nae kwenye basi au kwenye ndege au kwenye meli au barabarani ukitembea, ukiangalia kwa kina ni kama nguvu ya mahusiano inategemea sana na wapi mlianzisha mahusiano yenu. Wengine wana historia ndefu yaani wanakaa mtaa mmoja, wamesoma shule moja, wanasali msikiti au kanisa moja, wakasoma chuo kimoja. Mazingira yanayotukutanisha yana nguvu sana kwani swala hapo sio mazingira tu bali kuna vitu vya ndani yake.
Ndani ya mahali mlipoanzia safari kulikuwa na sababu, mfano kama mlikutana kwenye basi ina maanisha kuwa usingesafiri na basi au usafiri huo aliotumia na yeye ni wazi kuwa asingekuwa yeye
Kama ungekuwa mahali hapo nje ya muda ambao yeye yupo pia ni wazi kuwa angekuwa mwingine na matokeo mengine kabisa
Lazima mmoja wenu alitengeneza mazingira mazuri ya kuanzisha jambo ambalo kwa namna moja au nyingine liliwaunganisha na mkaanza kuwasiliana au kuongea na ndani ya muda mfupi mkajiona mmefahamiana sana
Ilitegemea sana hali uliyokuwa nayo au uliyokuwa unapitia na kwa namna moja au nyingine ulihitaji mazingira fulani ili uweze kujisikia vizuri
Kumbuka mambo haya yote yanatokea kwa wakati mmoja katika eneo ambalo linaanzisha safari ya ukaribu. Watu wawili wasiozaliwa tumbo moja na waliokutana tu kwa njia moja au nyingine mahali fulani ni lazima kuwepo na sababu ya kuwaunganisha. Hapa nitaelezea zaidi ukurasa unaofuata ila niseme kwa kifupi. Sababu ya kukutana ina nguvu kuliko mahali pa kukutana. Ni kwasababu hiyo ndio maana ilikuwa ni lazima mkutane hapo. Kusudi lina nguvu kuliko eneo au mazingira. Mazingira yapo kulitumikia kusudi. Mfano, mlikutana shule, sababu ya kukutana hapo ni kusoma, hiyo sababu ndio iliyopelekea mkutane;KUSOMA. Mngeweza kukutana kokote lakini ilibidi tu mkutane hapo kwenye hiyo shule, kumbuka kama ni wanafunzi wako wengi sana, kwanini yeye? Hapo jiulize. Kuna watu nisingeishi Dodoma nisingewafahamu kama ninavyowafahamu sasa pamoja na mambo mazuri yote na fursa walizozibeba ndani yao kwa ajili yangu. Mlikutania kwenye semina ya kiroho, fikiria kama usingeenda. Mlikutania chuo, fikiria kama usingechaguliwa chuo alichochaguliwa. Yaani ni lazima wewe na yeye muwepo MAHALI pamoja kwa namna yoyote ile. Hata kama ulipigiwa pande na kuunganishwa nae na mtu mwingine bado ni lazima LOCATION inadai haki yake.
Tafakari mahali ulipoanzishia ukaribu wako na mtu, kumbuka ukaribu alioupata kwa muda mfupi sana wa kuongea. Ukamfurahia. Ukaanza kusema yote yaliyo moyoni mwako bila kusahau kutweka mpaka kilindini. Ukaribu. Kwanini ulimuamini sana kwa muda mfupi hivo? Angalia, huwezi kulala bila kuongea nae, mnachat mpaka mnalalia usingizini na simu viganjani, cha ajabu kwakuwa wewe umekuwa mwepesi sana unasema vya moyoni mwako ni vile hujajua kuwa na yeye huwa anapata muda wa kuwaambia rafiki zake mawasiliano yenu yote. Hakika moyoni umo udanganyifu. NILIJIKUTA TU NIMEZOANA NAE. Kwanini ulienda?

Itaendelea.
Raphael JL:
Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428