Leo ni tarehe 31. 12. 2017. Muda huu naandika ujume huu ni saa sita na dakika kumi na saba. Niko nyumbani kwangu, Nkuhungu-Dodoma. Kuna hali ya mawingu ya mvua na huku najiandaa na mkesha wa mwaka mpya hapo baadae. Haya ni muhimu kuyajua.
Kuna mambo kadhaa napenda kuyasema huenda yakakusaidia kujifanyia tathmini na kujua uhalisi wa hisia na tabia zako. Siku ya leo ni siku ya mwisho kabisa kwa mwaka 2017 na haitajirudia milele na milele. Najua yako mambo mengi ambayo uliyapanga au kupangiwa kuyafanya kwa mwaka 2017 na leo ni siku nzuri sana ya kujikagua na kuona umeendaje. Zingatia kwa kujiuliza yafuatayo:
• Ulipanga nini
• Ulipangaje
• Ulipanga na nani
• Kwa nini ulipanga
• Ulipanga kwa muda gani
• Ulipangia wapi
Mipango na ufahamu
Ndio jiulize na ujikague. Mwaka huu wa 2017 ulipoanza ulipanga kufanya nini, ulipanga kwenda wapi, ulipanga nini kwa ujumla wake? Ainisha mambo uliyopanga na kama kweli ulipanga. Najua huwezi kujua kama ulipanga nini kama hakuna mahali uliandika chochote kuhusu Mipango Mipango hiyo. Kwa hiyo kama hukuandika chochote mahali popote basi liweke hilo kuwa kosa la kwanza ulilofanya lililokusaidia kufanya vibaya kwa mwaka 2017. Kosa lenyewe ni kutokuandika mawazo yako mahali Fulani ili iwe rahisi kuyafuatilia. Andika.
Katika kupanga inawezekana uliruka hatua. Huwezi kupanga kama huna Mipango. Mipango ni mkusanyiko wa mawazo. Mawazo ni mkusanyiko wa taarifa. Taarifa ni jumla ya mambo yote uliyoyasikia kabla na baada ya mwaka 2017 kuanza na ambyo ndiyo yaliyokusaidia kupatia au kukosea kuwa na mawazo yaliyokuwa Mipango ulokusudia kuyafanya kwa mwaka mzima wa 2017. Hapo yako makosa mengi ambayo huenda ulipatia moja na kukosea jingine na ndo maana upo hapo ulipo.
Tatizo sio kupanga tu. Ipo namna ulivyopanga. Na pia ulipanga nini. Kwa nini ulipanga hivyo na kwanini ulipanga hayo. Ulijuaje Mipango yako iko sahihi? Tafakari Mithali 16:1 inasema hivi;maandalio ya moyo ni ya mwanadamu, bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana, tafakari tena hilo neno. Inawezekana ulipanga kwani ulikuwa na Mipango yoyote. Inawezekana. Lakini kuna kosa jingine ulifanya. Uliamua kupanga peke yako. Yaani hukuona kama Mungu ananafasi kwenye Mipango yako. Kuna makosa yako pale juu ambayo sijayaweka vizuri hapa. Ngoja nielezee kidogo, najua utaelewa tu.
Nilisema, huwezi kupanga kama hauna Mipango. Hii ni muhimu sana kuelewa. Ukijikagua hapo ulipo inawezekana bado huna Mipango ya mwaka 2018 kama ukivuka kwa neema ya Mungu. Nikasema pia kuwa Mipango inazaliwa au inatoka ndani ya mawazo ya mtu, yaani mkusanyiko wa mawazo mbalimbali ndio unakuwa kama msingi wa kuanza kuwaza kupanga. WAZO LINA NGUVU KULIKO MPANGO. Ubora wa mawazo yako unatakiwa ukusaidie kuwa na Mipango mizuri, naamaanisha ubora wa Mipango na uzuri wake ni matokeo ya mawazo. Mawazo au fikra zako au matokeo ya mambo ulosikia na kuambiwa na kufundishwa mpaka yakaumbika ndani yako kuwa wazo kamili linalotakiwa kuandikwa na kufanyiwa kazi. Ninayoandika hapa ni mawazo yaliyofanyiwa kazi ndani yangu na yakathibitika na nikayaamini kuwa ni kweli na sasa nayatafsiri kwa kuyaandika ili na wewe uweze kuona uhalisia Zaidi tu ya kama yangebaki ndani yangu. Wazo zuri linahitaji mpango mzuri ili lizae matunda. Ndo maana nilisema wazo lina nguvu kuliko mpango, lakini wazo zuri likipata mpango mbaya pia ni sawa na kutokuwa na wazo kabisa.
Huenda ulikosea kuwaza. Ulikosea kuwaza na hiyo ikakusaidia kukosea kupanga. Ulipokosea kuwaza tu ikakusaidia kukosea kutafsiri ulichowaza na yote uliyoendelea kuwaza na mwishowe ukawa huwezi kupanga vizuri. Mipango mizuri inayopangwa na mtu aliyekosea kuelewa haiendi popote. Jipime. Kukosea kuwaza ni jambo kubwa sana. Kumbuka kusikia sio kuelewa. Kuelewa sio kufanya. Kufanya sio kupatia. Kwani sio wote waliosikia walielewa kama wewe. Sio wote walioelewa walifanya kama walivyoelewa na kwahiyo sio wote waliopatia. Jikague.
Tatizo la kukosea kuwaza au kuwaza vibaya inawezekana lilichangiwa na mambo ulosikia na namna ulivyoyasikia na ulikuwa kwenye hali gani wakati unayasikia. Na hapo ndo maana nilisema mawazo ni mkusanyiko wa taarifa ulizoruhusu kusikia au kuziona na kuzitafsiri na kuzipokea ndani yako. Hayo ndo mawazo yako kwani Mithali 23:7 iko wazi sana kusema;aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo…
Kwa hiyo maswali ya kujifanyia tathmini yanaweza kuwa kama ifuatvyo na yote yapatie majibu usiishie kuyasoma;
1. Mwaka 2017 ulipokuwa unaanza wewe ulikuwa na ufahamu wa namna gani au taarifa zipi ulikuwa umezipata zilizokusaidia kupanga kama ulipanga?
2. Kwanini ulipanga Mipango uliyopanga?
3. Kwanini uliipanga Mipango kwa namna ulivyopanga?
4. Kama uliweka Mipango na hukuifanyia kazi, kwanini uliiweka na kwanini hukuifanyia kazi?
5. Kama uliifanyia kazi na haikufanikiwa, jiulize kwanini?
Ukisoma kwa makini hapa utagundua kuwa ninachozungumzia ni Zaidi tu ya kuwa na Mipango. Ninazungumzia pia NIA iliyokuwa nyuma ya Mipango uliyojiwekea mwanzoni kabisa. Nia ya kuwa na mipango inatakiwa iwe kubwa kuliko changamoto zote utakazokutana nazo mbele yako. Kwanini watu huendelea na masomo hata ikiwezekana kurudia mitihani ili mradi tu aendelee mbele? Nia ikizidiwa na changamoto au starehe basi ujue utaishia kusimulia na kuyatamani mafanikio yaw engine milele.
Mipango na nia
Nia ni mkusanyiko wa mawazo unaokufanya au kukusababisha ufanye lolote unalotaka kulifanya kwa nguvu na Imani kubwa. Nia ni nguvu ya kukusudia iliyo nyuma ya kila jambo unalofanya au unalokusudia kufanya. Nia ni ushawishi wa ndani unaompa mtu nguvu na motisha ya kuamua kufanya jambo lolote bila kujali vitisho au changamoto zinazotokana nay eye kulifanya jambo hilo. Nia iko moyoni. Nia hubadilika kutegemeana na mambo mawili makubwa:
1. Nguvu ya ushawishi
2. Nguvu ya changamoto
Nia ni sababu nyuma ya tendo unalofanya. Swali linalozaa nia ni KWANINI. Yes, kwanini ulipanga mipango kama hiyo? Ulitaka usifiwe au uonekane na wewe una mipango? Shika hili, kuwa na sababu mbaya au nia mbaya kufanya jambo lolote ni sawa na kupanga kukosea mwisho wa jambo maana mwanzoni utaona uko sawa. Nia mbaya ya kufanya jambo haiwezi kuzaa matokea mazuri ya jambo husika. Nia ya shetani kwenye maisha ya mwanadamu ni kuchinja, kuua na kuharibu. Nia yake nii imefichwa ndani ya mioyo ya wanadamu ambao huwa wana nia mbaya (kuchinja, kuua au kuharibu au vyote kwa wakati mmoja). Nia ya Yesu Kristo ni kuwapa wanadamu uzima toshelevu, yaani uzima teletele. Wapo wanadamu walioibeba nia ya shetani na wapo walioibeba nia ya Yesu ndani yao.
Nilisema hapo juu kuwa nia hubadilika. Na nikasema nia hubadilishwa kwa mambo makubwa mawili. Huenda yapo mengine lakini nataka ujitathimini kwa haya mawili halafu ukusudie jambo jipya mwaka 2015. Tegemeo langu ni kuwa kwa wewe kuyajua haya maeneo mawili itakusaidia kutokuturudia kosa lilelile ulilokosea mwaka 2017. Hebu ngoja nielezee kidogo.
Nguvu ya ushawishi
Mithali 1:10;mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe Usikubali. Pia soma Mwanzo 3:6, inasema Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Kwa uchache wa maeneo hayo mawili napenda nieleweke vizuri. Nilisema kuwa nia hubadilika. Nia inapobadilika hubadilisha na vyote vilivyo ndani yake ikiwa ni pamoja na mawazo na mipango yake. Nia inabadilikia ndani ya mtu na sio nje ingawa nia hubadilishwa Zaidi na mambo yaliyo nje ya mtu. Inawezekana ulibadili mawazo na mipango yako kwa kusikia au kuona. Ulioona na kusikia ukaanza kuwaza na kupima uliyoyaona na kuyasikia ukilinganisha na uliyokuwa unayajua awali, na mwishowe ukaamua kubadilika.
Ushawishi una nguvu sana. Namaanisha ipo nguvu au matokeo mazuri au mabaya ya kushawishiwa au kushawishika. Unaweza kushawishiwa kwa ubaya au uzuri, ni muhimu kuwa mwangalifu na kupima aina ya ushawishi unaokuja kwako kabla hujakubali. Wenye dhambi wakikushawishi Usikubali. Nini maana ya ushawishi? Kushawishi ni kutumia lugha ya picha au maneno ya kawaida lakini yenye nguvu ya kumfanya mtu aone anachojua kuwa si sawa kinaonekana sawa na kinyume chake. Kumshawishi mtu ni kumsaidia kuwaza kinyume na anayoyajua nab ado asione kama ni kosa. Mtu anaweza akakushawishi kwa kukuonyesha kitu na wewe ukaona kwa macho yako na ukashawishika kutokana na kiwango cha ufahamu wako juu ya jambo husika. Kwa mfano Adam na Eva pale bustanini. Kilichomshawishi Eva kula tunda ni kwasababu lile ule mti wa matunda waliokatazwa kula:
1. Wafaa kwa chakula
2. Wapendeza macho
3. Unatamanika kwa maarifa, AKALA na akampa na mumewe naye AKALA.
Jipime. Ni mambo mangapi uliamua kuyafanya au kutokuyafanya ambayo yalisababishwa na nguvu ya ushawishi, aidha ulishawishiwa kwa maneno mataamu kama yale ya nyoka na ukajikuta umeamua kula. Hukula peke yako. Maamuzi hayo ya kuacha mipango ulokuwa nayo kwa mwaka 2017, ukaamua kufanya mawazo ya watu wengine kwa ushawishi wao yamekuathiri wewe pamoja na watu wanaokuzunguka. Ushaiwishi una nguvu sana kwasababu hufanywa na watu wetu wa karibu aidha kwa kutumiwa au kutumika wao wenyewe. Kumbuka Eva hakushaawishiwa kwasababu alikuwa na njaa. Hapana. Alikuwa na sababu zake kama nilivyokuonyesha hapo juu.
Nguvu ya changamoto
Esau alikuwa na njaa sana. Amehangaika na mawindo kutwa yote na hajapata. Ana njaa ambayo kwake ingeweza kumuua. Akamfanta mdogo wake aitwae Yakobo. Yakobo alikuwa na chakula. Kumbuka pia Daniel pia alikaribishwa chakula na Mfalme Nebukadreza (Daniel 1:8). Eshau aliuza haki yake ya uzaliwa wa kwanza (aliuza hatma yake au destiny) na kuharibu mipango yote ya maisha yake kuanzia muda ule. Daniel yeye alikataa kuuza hatma yake kwa chakula. Inawezekana. Ulikuwa na mipango mingi na mizuri kwa mwaka 2017 lakini iliharibiwa na offer za vitu kama vyakula ulivyopewa. Zawadi ulizopokea. Labda hudhani kama chakula kina nguvu na ndo maana unakula tu bila kujua kua nia ya aliyekupa chakula inatimia kwa wewe kukubali kula. Au kuna changamoto nyingine za maisha zilizokufanya ukabadilisha nia ulokuwa nayo ya kufanya vile ulivyokuwa umekusudia.
Swali la msingi: kwanini hukufanya ulotakiwa na kukusudiwa kuyafanya mwaka 2017 na leo ni tarehe ya mwisho kabisa ya mwaka huu?
Hapo juu nimejaribu kukuelezea upande wa muhimu wa labda ulipanga lakini kwanini uliyoyapanga hayakufanikiwa. Japo kwa kiasi lakini naamini kuna kitu umejifunza cha kukusaidia kwa mwaka 2018.
Mipango na marafiki
Huenda ni aina ya watu ulioamua kutembea nao mwaka 2017 ndio sababu ya kusuasua na kufika hapo ulipo. Ukitembea na mwenye hekima lazima na wewe utaambulia hekima. Wapo watu aina mbili. Upande mmoja una watu wanaokusaidia kufanikiwa kwa nia njema kabisa na upande mwingine una watu wanaokusaidia kukosea kwa hiari yako mwenyewe. Kuna jambo nataka ulifanye kwa kumaanisha kabisa mpendwa. Kagua, kwa mwaka 2017 andika pembeni watu wote unaokumbuka wamekusaidia kupatia na kupiga hatua na kuendelea mbele na kukua Zaidi na kuandika Zaidi na kuimba Zaidi na kuwa mtakatifu Zaidi na kuwa bora ziaidi, watu walioongeza thamani ya ufahamu wako. Waolodheshe maana wengine utawahitaji 2018 na wengine unatakiwa uwashukuru kwa kukusaidia kuwa nawe na kukufikisha hapo. Waolodheshe maana Mungu aliwatumia kukutoa matongotongo na kukunawisha na kukupa ufahamu ulokuwa unauhitaji hata wakati wewe hujui. Kumbuka Daud na Yonathani. Pia andika wale waliokusaidia kukosea na ukumbuke wealikusaidiaje maana mwaka 2018 watakuja na gia mpya na lengo lao ni lilelile la baba yao, kuchinja, kuua na kuharibu. Marafiki aua watu wa karibu tunaowaruhusu kuwa sehemu ya hisia zetu wana nafasi kubwa sana ya kuathiri hatma yetu.
Mipango na uzembe
Wapo wanaosota siku ya mwisho kwa mwaka 2017 kwasababu walifanya uzembe. Walifanya kwa ulegevu. Walijifanya wasahaulifu. Hawakuwa makini. Hawakuandika. Hawakufuatilia. Walichoka njiani. Waliona muda bado upo, wapuuziaji. Waliona sababu wanayo, wapenda raha. Waliona wataendelea kuishi. Wazembe. Wavivu. Bado kulala kidogo. Giza bado halijaisha. Na sasa wanagundua mchana umeendelea sana na mwaka unafungwa leo. Majira mapya. Kiriba kipya. Mvinyo mpya.
Mipango na nguvu ya kuona
Lutu aliona. Ibrahimu alionyeshwa. Elisha aliona. Mtumishi wake alifumbuliwa macho. Eva aliona. Esau aliona pia. Isaya aliona. Lutu aliona, akaishai Sodoma na Gomora. Punda aliona akasimama. Balaam hakuona na akampiga punda. Uonavyo nafsi mwako ndivyo ulivyo. Swali rahisi sana, uliona nini ulipokua unauanza mwaka 2017? Unaona nini unapoingia mwaka 2018? Si unajua kuna utofauti kati ya JICHO SAFI NA JICHO BOVU? Mathayo 6:22-23. Jicho chafu linasafishwa. Jicho bovu linatengenezwa. Huenda uliona lakini ukatafsiri vibaya, yaani ukatafsiri kama vile ufahamu wako ulivyokuwa. Kama uliishi maisha magumu huko nyuma, hisia zao zikakusaidia kutafsiri ugumu wa kila fursa uliyoipata. Hata wakati alipokuja mtu sahihi wewe ukatasfiri kusalitiwa maana ulishasalitiwa. Wakati wewe unajiona panzi, wapo wanaokuona mkubwa kuliko panzi. Mungu akamuuliza Yeremia, UNAONA NINI? Na alipoona na kusema aliambiwa ameona sawasawa. Uliona nini 2017? Unaona nini 2018? Kuona kunakupa kumiliki. Kuona kunakupa utayari. Kuona kunakufanya uwe wa tofauti. Kama jicho lako ni chafu litakase kwa NENO LA MUNGU. Ni jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Ukienda gereji na gari ambayo ni chafu nan i mbovu pia, fundi wa ukweli hawezi kuanza kuisafisha gari kabla ya kuitengeneza. Mruhusu Roho Mtakatifu akutengeneze le oleo tena. Usisubiri mkesha maana unaweza usifike. Fanya sasa. Amua sasa.
Mipango na maamuzi
Ulikuwa na mipango. Ukaiandika. Ukaiombea. Ukaifurahia. Ukaisema kwa watu. Kila ukifungua diary unaisoma na inakuhamasisha kuongea na kuwaza Zaidi. Ukawaza Zaidi. Ukahamasishwa Zaidi. Basi. Hukuendelea Zaidi. Hukuamua. Hukuamua kuamua. Hukuamua kulipa gharama. Ulidhani wapo watu wanatakiwa walipe gharama kwa niaba yako kwani wewe ni wa pekee sana. Ulianza kutoa visingizio. Mtaji mdogo. Itakuwaje na mimi niko kijijini. Sina elimu. Ukajidanganya. Ukasubiri malaika washuke wakusaidie kuamua. Ukabaki kuwa shabiki. Ukabaki kuwa mfuasi wa walioamua kuamua. Mpaka leo tarehe 31.12.2017 unajishangaa umewezaje kufika mwisho wa mwaka. Ni bora usiwe na mipango kuliko kuwa nayo na kushindwa kuitekeleza. Ni bora kutokujifunza kuliko kujifunza na kuendelea kuwa mpumbavu. Maajabu ni kwamba unashauku ya kuvuka kwenda mwaka mwingine na huku una furushi la viporo vya kutokuwajibika mwaka 2017. Una furushi la kijitetea kutokuwajibika la mwaka 2017. Una kiporo cha uzembe. Kiporo cha uzurururaji. Una furushi la kukwepa majukumu mwaka 2017. Jiulize, mwaka 2018 utaweza? Wakati wenzako wanakua kwa kwenda mbele, wewe unakua kwa kubaki hapo ulipo, bora ungerudi nyuma kidogo. AMUA KUAMUA. Acha kujihurumia kama unataka ufanye kwa ubora. Wewe si wa kwanza kukosea. Hautakuwa wa mwisho. Jaribu. Fanya.
Mipango na YKM
YKM tumeweza kufanya event tofauti tofauti 19 na Zaidi kwa mwaka 2017. Huenda wewe unaesoma ni mmoja ya watu walioguswa na hayo tulofanya kwa mwaka 2017. Huenda ulipata jumbe zinazotumwa na huduma mbalimbali za YKM. Huenda ulipata jumbe za nukuu ya Raphael JL: huenda. Nawaza, ingekuwaje kama tusingefanya. Kama tusingekubali. Kama tusingekuwa tayari. Kama usingeamua kufanya? Tunauangalia mwaka 2017 kwa YKM kama mwaka ulotufundisha mengi. Katika yote nia ni ile ile. Tumeona mengi. Tumesafiri mpaka Ruvuma. Kilimanjaro. Arusha. Dar es salaam. Dodoma. Morogoro. Singida. Mbeya. Africa ya Kusini. China. Marekani. Kenya. Uingereza. Lindi. Mtwara. Mwanza. Swaziland. Tumeona vijana wakibadilika. Wakimjua Mungu. Wakiipenda Tanzania. Tegemea Zaidi mwaka 2018.
Jesus Up-YKM.
Mungu akuinue kwa kuyasoma haya. Mungu akupe neema ya kufanya vizuri mwaka 2018. Mungu akuponye na yaliyotokea mwaka 2017. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikufunike. Upendo wa Mungu Baba uwe fahjari yako. Ushirika wa Roho Mtakatifu uwe kiu yako.
ONE STEP AT A TIME.
By Raphael Joachim Lyela
YKM Founder
Dodoma-Tanzania-East Africa.
Email: faryesu@hotmail.com
Phone: 0767033300