Mungu kwanza

Saturday, 30 December 2017

MPUMBAVU KATIKA UBORA WA UPUMBAVU WAKE

                                 MPUMBAVU KATIKA UBORA WA UPUMBAVU WAKE


Mjinga ni mtu asiyejua na mara nyingi anaweza asilaumiwe ingawa himfanyi kuepuka adhabu kama atakosea kwa ujinga wake. Mjinga dawa yake ni shule ilia pate ufahamu na akipata ufahamu basi ujue ameshinda. Ujinga ni moja kati ya maadui watatu wakubwa waliotangazwa na baba wa taifa, mwl JK Nyerere na ndo maana ni kila mtu anatakiwa apelekwe shule ili akapate ufahamu unaoweza kumsaidia mtu. Inaaminika kuwa mjinga akielimika basi kiwango cha umasikini pia unapungua. Kaka ake na mjinga anaitwa mpumbavu. Upumbavu ni hali, sio tusi. Mpumbavu ni mtu. Mpumbavu ni mtu alievuka kiwango cha kuwa mjinga, yaani akapata maarifa na akavuka toka kwenye ujinga na akawa mtu mwenye uelewa. Utofauti kati ya mjinga na mpumbavu ni utekelezaji. Kumbuka si kila anaesikia anaelewa, si kila anaelewa anafanya na si kila anaefanya anapatia. Kumbe mpumbavu ni mtu anajua na hafanyi anachokijua. Upumbavu ni hali ya kujua jambo na kutokulifanya kama unavyolijua.

Mpumbavu katika ubora wa upumbavu wake hujua mengi na kujisifia anajua na hatekelezi hata moja kati ya anayojua. Upumbavu hauna mtaala. Namaanisha upumbavu wa mpumbavu hauishi kwa kupelekwa shule kwani hakuna shule ya kukufundisha kufanya unayojua zaidi ya kuamua kufanya. Wajinga ni wachache sana. Wapumbavu wanaweza wasihesabike. Ni vigumu kukubali kama mimi ni mpumbavu lakini kwakuwa leo nimekusudia kuvuka hili eneo na kufichuliwa basi niko tayari hata kama ni kwa maumivu. Mpaka hapa najiona na maupumbavu yangu. Kipimo cha upumbavu wenye ubora ni rahisi sana maana kuna jambo moja tu la kujiuliza na ambalo kama unajipenda ujajibu bila kuigilizia kwa yeyote.

Najiuliza, nimefundishwa kumtolea Mungu na ninaamini kuwa ni jambo jema lakini sitoi maana naogopa kufilisika na huku nawaza nikitoa nitapungukiwa ingawa najua dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Mimi ni mpumbavu,asante. Ninajua kabisa kufanya jambo fulani ni sawa na haki lakini sifanyi. Nimeandika notes nyingi sana za mafundisho lakini kiwango cha maisha ninayoishi hakilingani wala kufanania na mambo ninayoyajua. Najisifia na kujivunia kwa kuhudhuria semina, na kuwashangaa wale ambao hawakuudhuria ingawa kwenye maisha halisi wao wanaenda vizuri kuliko mimi, mimi nina notes na wao wana vitendo. Mimi sio mjinga. Mimi ni mpumbavu. Ni mtu ninaejua lakini sifanyi. Zipo sababu nzuri zinazonisaidia kutokufanya lakini kubwa kabisa ni upumbavu wenyewe.

Ninajivuna kumjua Mungu lakini siko tayari kuwasamehe walionikosea kama ninavyojua maana kuwasamehe hivihivi inauma bila kuwatukana au kuwarudishia hata kidogo na hasa kama walifanya makusudi kabisa kuniumiza. Ni kweli najua natakiwa kusamehe lakini kuna watu ukiwasamehe watajiona sana na wewe utakuwa masikini sana. Mimi ni mpumbavu. Zaburi 14:1, mpumbavu amesema moyoni, hakuna Mungu; wameharibu matendoo yao na kuyafanya chukizo, hakuna atendae mema. Akishaamini hakuna Mungu basi kila analofanya litathibitisha hakuna Mungu ingawa anajua kabisa kuwa Mungu yupo ila kwakuwa upumbavu uko kwenye ubora wake basi anajisikia vizuri kwa muda huo. Nataka niache kuwa mpumbavu.

Nimekusudia kuacha upumbavu. Niko tayari kulipa gharama. Eee nafsi yangu kubali kubadilika maana haifai kujisifia mambo mazuri ninayoyajua nisiyoyafanya. Kwanini nijisifie kusoma vitabu 10,000 na ninaishi maisha ya kitabu kimoja, sitaki kujikatisha tamaa kusoma vitabu ila nataka nisome with substance. Kama nimeokoka basi maisha yangu yawe nuru kweli kweli na sio kuwafanya hata wasiookoka watamani kurudi nyuma kwasababu siishi kama mtu ninae amini. Leo naacha uganga huu na upumbavu wake. Kwanini nifundishe wengine mabadiliko na mimi mwenyewe ni afadhali na wao. Nimewezaje kujua bila kuyaishi?

Wengi huenda shule na kupata elimu bila ya wao kuelimika. Wengi kuenda kanisani kama wahuduriaji na wachache kushiriki na kubadilishwa. Wengi husema wameelewa lakini matendo huwa hayaonekani kuelewa kwao. Na mimi sitaki niwe mmoja wao. Upumbavu ndani yangu, shindwa na ulegee uwe kama mlenda. Sitaki kuwa mpumbavu. Nimefundishwa kujizuia, mbona ndo nazidi kujiachia? Nimefundishwa kutokuwadharau wengine, mbona nazidi kujiinua. Haiwezekani. Niko tayari kufichuliwa. Niko tayari kufichuka. Najiuliza, kwanini nipambane kujiuliza kama nitoe fungu la kumi gross au net na ninaemtolea ni Mungu ambaye ndani yake ninaishi, ninaendenda na kuwa na uzima wangu? Ni nini ndani yangu ambacho si mali yake? Nakumbuka ninaimba ule wimbo, yote namtolea Yesu lakini kuna mambo mbona bado naona anataka kunifilisi kijanja? Leo sikubali. Mungu wangu nifungue kabisa.

Nimekaa nikawaza katika ule upumbavu wangu wa mpumbavu ajuae kila kitu nikaona niandike hili maana najua kwa kuwandika nabadilika na kuwa mwelewa mtekelezaji maana kwa Imani yangu pia najua na ninaamini kujua jambo jema na kutokulifanya sio tu ni upumbavu bali ni dhambi. Basi nimevuka. Najikagua, mangapi nayajua lakini siyafanyi, naanza upya. Nimefichukaa hata kama ni kwa maumivu. Mungu wangu naomba unisaidie na umsaidie rafiki yangu asomae hapa pia. Wapumbavu hulalamikia hadi vitu ambavyo wanaweza kufanya lakini hupenda kuwalaumu wengine maana wako katika ubora wa upumbavu wao. FICHUKA.
Raphael JL
YKM Founder.
Dodoma-Tanzania.
Jesus Up
Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428