Mungu kwanza

Saturday, 30 December 2017

ANZIA ULIPOISHIA-KUSANYA NGUVU YA KUENDELEA



Vipi kama hujawahi kuishia popote, ina maana hukuwahi kuanza popote na kwa hiyo anzia ulipo. Inawezekana unasoma hapa huku una maumivu ya kukwama katika ndoto au mawazo au mipango au mikakati au maono yako au kanisa lako au ya familia yako. Inawezekana kabisa kuwa huduma inaoneka haindi popote zaidi ya nyuma na unatamani hata ingekuwa heri kama ingesimama tu kuliko kurudi nyuma. Ukweli wa mauimivu haya unachangiwa na kiasi cha nguvu ulizowekeza kwa Imani katika eneo husika. Uliamini angekuwepo aliyekuelewa mwanzoni ili akusaidie kipindi hiki cha mpito lakini na yeye akawa yuko njiapanda ya maisha yake kwani hajui nini anatakiwa kufanya.


Unawaza kiasi cha jitihada na pesa ulichotumia na kudhani mambo yangekwenda kama ulivyoambiwa au ulivyoona lakini yakakwama. Upo unaogopa kuanza kufanya maana umezungukwa na makosa kwa kiwango ambacho na wewe unajiona si tu kuwa utakosea bali tayari ni mkosaji. Unaogopa kuchukua hatua nyingine kwani unaona huwezi hata kuinua mguu na kuanza kwa hasara uliyoipata mpaka hapo ulipofikia. Ulianza shule ukiamini utafaulu na kuendelea mbele zaidi lakini sasa upo hapo na huna uhakika wa kumaliza kwani ada hujui itakuwaje. Uliamini wazazi wako ndo mwisho wa mambo yote na sasa uko njia panda maana wote wamefariki na hujui unaanzaje kushi ukiwa na uhuru wa kuamua na kujitegemea mwenyewe. Umekaa na huamini macho yako kwani unajiuliza nini maana ya kuwa na wazazi kama huoni msaada wao na ungetamani ujue kwa nini.


Moyo mmoja unawaza mengi maana yote yanagusa maisha, vipi kuhusu marafiki ulowaamini sana na huoni kama kunai le nguvu. Ulijaribu mara ya kwanza wakakuambia hukuumbiwa hilo unalojaribu na kwahiyo tafuta namna nyingine. Ukakaa nao mbali na kimsingi hukuwa na nguvu tena ya kusimama na kufanya kwani ukagundua adui zako ni watu wa karibu yako zaidi ya unavyojiamini. Ukakata tamaa. Ukachoka. Ukaacha. Ukatupa. Ukaficha. Ukajificha. Ukajiweka na kujitenga mbali. Ukawa hujui unafanyaje na unaendeleaje kutoka hapo ulipo. Ni kweli kwamba sijui ulipo ila najua upo mahali fulani na nataka niongee na wewe ukiwa hapo ulipo yaani hapo hapo ulipo.


Nataka niongee na wewe sio tu hapo ulipo bali pamoja na hali uliyonayo maana vyote viwili ni vya muhimu kwa jambo hili. Iwe ni mahusiano au biashara au nyumba au ndoa au huduma au kazi au mipango. Hapo hapo ulipo na hali ulonayo. Vuta pumzi,pheeeeew. Kama ulianza ujue ina mwendelezo. Kama ulifanya ujue inawezekana. Ulianza ili uishie njiani? Kama jibu siyo sasa hapo umekaa na kuacha ili ujikomoe? Lazima ujue kuwa kushindwa sio kutokuweza na ukishindwa haimaanishi haiwezekani. Kaa chini ujichunguze na utagundua kuna mahali wewe ulichangia kukwama kwako. Ukigundua ni wewe basi jiongeze ili upanuke katika kuanza upya. Hivyohivyo ukigundua si wewe jiongeze kwa uoande huo huo. Lakini mimi nataka nikwambie neno moja tu ANZIA ULIPOISHIA.
Zaidi tembelea
Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428