Mjinga akienda shopping kwenye super market basi ujue siku hiyo wahudumu watakuwa na kazi sana ya kuulizwa maswali maana yeye atauliza maswali ya kuvishangaa vitu maana haivijui, hivyo atauliza sana ili ajue ndipo aamue. Ni wajinga wachache sana ambao akienda shopping ataanza kununua vitu hata kama havijui na mwishowe atanunua pipi akidhani ni goroli au sabuni ya unga akidhani ni unga wa kula. Sina hakika, lakini naamini inawezekana kabisa mtu akawa mjinga mwenye kiwango fulani cha upumbavu kwani mjinga ni mjinga kwa yale asiyoyajua tu, na kwa yale anayoyajua na hayafanyi basi ni mpumbavu.
Mpumbavu akienda shopping, hatawasumbua kabisa wahudumu maana kikawaida yeye lazima atakuwa anajua mengi kuliko wauzaji na anaweza kabisa akawasaidia hata kupanga bei. Kuna maduka ambayo ukiingia huwezi hata kusema nipunguzie kwani viwango vyake ni vya watu wasioweza kulalamikia bei ya kitu. Mpumbavu akienda shopping katika kiwango chake cha ujuaji basi atakuwa tayari kukosea kuliko kuuliza kwani hapendi kuonekana hajui.
Mpumbavu na mjinga wakipotea, kuna uwezekano wa mjinga kupata msaada kwa wepesi kuliko mpumbavu kwani kikawaida katika ule ubora wake mpumbavu anajua yote asiyoyafanya na kwa hiyo kuanza kuulizauliza ni kijishushia hadhi na ataonekana mshamba nay eye hataki. Mupmbavu akipotea huzidi kupotea zaidi maana kupotea kuna raha yake maana unajisikia tu kuendelea kwenda ukiamini utapata njia sahihi. Mpumbavu hudhani, wakati mjinga huuliza.
Mpumbavu kanunua simu mpya, basi mpaka kanisani kwenye ibada malaika watajua kuwa jamaa amevuka level moja kwenda nyingine. Sina haja ya kubeba biblia maana ninayo kwenye simu. Data bundle on maana biblia yangu sio offline enabled. Hapo hapo, facebook on, whatsapp on, viber on, Instagram on ila ringtone silence ili kutokuwasumbua wengine isipokuwa moyo wangu mwenyewe. Ninasoma biblia ya kwenye simu all the time, napangusa tu na kufuta tu na kumbe nimeshahama zamani sana na sasa niko kwenye kuangalia picha za last event, narudia kucheki msg za last conversation, yaani nimezama sana ndani kwa kiwango ambacho Mchungaji ananiita ili nisome kifungu fulani cha biblia na ninapata aibu ya mwaka. Najua kabisa kuwa naenda kwenye ibada.
Najiuliza kwanini najua haki lakini siitendi? Kwanini najua njia lakini siipiti? Kwanini najua jema na silitendi? Kwanini najua lakini naishi ujinga au upumbavu? Kwanini napenda tu kusikia lakini nashindwa kufanya ninayosikia? Kwani nikienda shopping na nikawa nawauliza wauzaji napungua uzito? Simu yangu, ibadani ninayo, njiani ninayo, kitandani ninayo chini ya mto. Ni bora nisijue ili nibaki kuwa mjinga ingawa ujinga sio tiketi ya kufanya mambo ya ajabu. Sitaki tu kujua na kujisifia ninajua wakati najua ni akili zangu tu maana mimi kama mpumbavu napenda sana kuzitegemea akili zangu. Ee Mungu nisaidie mimi na wale walio kama mimi katika upumbavu wetu, utuamshe hata kwa kutumwagia maji baridi.
Raphael JL