Mungu kwanza

Friday, 22 December 2017

UMAARUFU SIO KIPIMO CHA USAHIHI



UMAARUFU SIO USAHIHI, UZURI SIO KIPIMO: ADUI WA KUDUMU NI SHETANI TU HATA KAMA AKIWA NDANI YA UBORA

Nani kasema? Nani kapima? Nani kaanzisha? Nani kapitisha? Kwamba jambo likifanywa na mtu maarufu basi liko sahihi? Kwamba mtu maarufu akivaa nguo za virakaviraka kwake inakuwa fasheni, na kwako je? Nani kakubaliana na hayo? Kwamba mtu maarufu akikosea anakuwa kapatia? Kwamba mtu maarufu akivaa vibaya ni mtindo mpya mjini? Nani kasema? Mtu maarufu akienda eneo lisilo sahihi, akaenda kwenye madhabahu za baali na Ashtoreshi na kufanya ibada pamoja na wana wa uasi inakuwa sahihi?

Kwani uzuri ni nini? Kwani kujulikana ni nini? Kwani umaarufu ni nini? Na wala sijasema kuwa umaarufu au uzuri ni jambo baya ila nasema UBAYA UKO NDANI YA MTU, wote wawili, mtu anaeona na mtu aneoonwa. Ni aibu sana kuwa maarufu na huna hela. Ni aibu sana kuwa mzuri na una tabia za ajabu ajabu. Hakuna unafuu. Uchunguzi wangu kwa watu maarufu wanaoshi Marekani unaoneysha kuwa wanaishi maisha ya ucheshi na furaha na amani na kucheka sana wakiwa kwenye PUBLIC SPOTLIGHT yaani wakiwa wamezungukwa na mashabiki kwani umaarufu ni ushabiki kwa kuanzia.

Watu hawa maarufu sana dunia nzima, hakuna asiye wajua, wana maisha ya kifahari sana kwa kila aina ya starehe waitakayo iwe ni kwa wanaume au wanawake na mali na utajiri na kumiliki majumba ya kifahari sana. Nilipofuatilia kwa ukaribu nikaona UTUPU NA UPWEKE walionao wakiwa peke yao. Wakiwa hawaonekani tena ili kupiga picha na mashabiki wao, wakiwa huko kwenye maiha yao binafsi ya kukaa bila mtu wa kukusifia na kukwambia wewe ni mzuri au unatisha sana. Ni wapweke sana. Sana.

Nikafuatilia zaidi kwa uwaangalia waimbaji kadhaa wa kimarekani, nikashangaa sana kwamba hata nyimbo wanazoimba nyingi zimejaa malalamiko ya kufungwa na kukandamizwa na ni kama hawana la kufanya na wala hawawezi kutoka. Mashairi yao yamejaa maumivu ya kuonewa na kukandamizwa na mifumo inayotoa pesa na kuwapa nyota ya kukubalika ila kwa gharama ya maisha yao na ya uzao wao ikibidi. Nikaangalia kwa wale ambao wameshakufa, namna walivyokufa na jinsi walivyoacha gumzo la SINTOFAHAMU ya maisha yao.

Wapo waliokuwa matajiri sana ila sasa hawana kitu, ila sasa wana madeni ambayo hawawezi kuyalipa hata iweje maana wengi walinunuliwa na mifumo inayotengeneza TUZO za mashindano. Walipopewa tuzo wakajikuta wameingia kwenye mifumo migumu sana yenye uharibifu wenye rangi nzuri sana kwa nje lakini ndani yake una meno ya chuma na ulimi wenye kutu jingi. Wengi wanajitahidi kutoka lakini wanashindwa kwani maisha wanayoishi, ya ufahari yana masharti magumu sana ya mauti.

Hawa ndio ambao wakifanya kitu kinaonekana sawa kisa tu yeye amefanya lakini ndani yake anashindwa namna ya kujiengua. Wapo wanoataka kuwa maarufu, vijana wa leo, wakidhani kuwa umaarufu ndio HATMA YA MAISHA YAO na kwa hiyo wako tayari kufanya lolote ili tu wafahamike kwani kuna hela nyingi zimewekwa kwenye kutengeneza matangazo ya biashara na kwenye mashindano yanayotoa TUZO ZA UWEZO wa mtu. Kama umaarufu ukiwa ndo usahihi, na huku watu maarufu ni wachache sana duniani, inamaanisha watu wasio maarufu hawana wanachofanya duniani. Hata hivo, kila mtu ni maarufu kwenye eneo lake, ila mimi siongelei kiwango cha eneo lake, naongelea kiwango chenye ushawishi duniani.

Umaarufu sio mbaya ila ukitengeezwa unaweza kuwa na kusudi lake pia. Na ni lazima utengenezwe. Lazima uandaliwe. Kwani una ndoto ya kuwa MWANAMITINDO MKUBWA DUNIANI au unataka kuwa MISS HEAVEN au unataka kuwa nani sijui. Ukiangalia kwa makini utagundua kitu cha ajabu sana kwamba UMAARUFU UMETENGENEZEWA NJIA YA KUPITA NA MIFUMO YAKE TAYARI. Yaani huwezi kuwa maarufu bila kufanya vitu fulani au kwenda mahali fulani au kukutana na watu fulani au kuvaa namna fulani na kuongea namna fulani na kupewa tuzo fulani hivi.

Mahangaiko ya mtu maarufu au mtu mwenye uwezo sana na anaejulikana sana ni makubwa sana kama hajakaa vizuri kwani watu wengi wana namna hii huwa hawana marafiki wa kweli kivile. Na maisha yao ya kijamii ni ya kuigiza sana. Ni kama maisha ya watumishi wa Mungu, mduara ni ule ule tu, maisha ya kijamii yanakuwa mbali sana labda siku za harusi na sikukuu. Mduara umejifunga. Hivyo hata akiwa ana changamoto fulani hawezi kuisema au anawaza ataisema kwa nani ili ASISHUSHE JINA LAKE. Na kwahiyo anakaa kwenye kificho cha mambo yake akitafunwa sana ndani ya nafsi yake. Ghafla unasikia mtu amejiua, au amekufa ghafla au ameanza kufanya vitu vya ajabu tu.

Nimemfuatilia kwa muda mrefu R-Kelly na maisha yake, alivyokuwa na alivyo sasa. Majuto yake na masikitiko hata kwenye nyimbo zake, nini kiliua urafiki wake na Jay Z. Nimemuangalia Michael Jacskon, nikajifunza kitu kwa Kirk Franklin na Don Moen, bila kusahau alivyo sasa Kanye West na Ron Kenoly. Na Whitney Houston na mwisho wake, nikamkumbuka Brenda Fassie na Beyonce. Kwa mbali namkumbuka Tupac na Big. Hawa ni baadhi ya watu mashuhuri na maarufu sana duniani. Wanaheshimika sana. Wanaigwa sana. Wanakubalika sana. Lakini kuna mengi ya kujifunza katika kupatia na kukosea kwao.

Tujifunze. Tujipime. Tujikague. Kabla hujaiga kitu, kabla hujavaa anavyovaa mtu maarufu anaekugusa kumbuka hata wewe unao UTAMBULISHO WAKO. YESU KRISTO NI BWANA.
Share:

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428