Mungu kwanza

Sunday 3 March 2019

KUTEMBEA NA MUNGU MWENYE NGUVU HALAFU WEWE HUNA

KUTEMBEA NA MUNGU MWENYE NGUVU HALAFU WEWE HUNA
Jesus Up!
Napenda mwaka mwaka huu nitembee na nifanye kazi na Mungu na tena nifanye kazi zake na tena kwa utukufu wake, yaani ili yeye asifiwe na afahamike zaidi kupitia kila jambo nitakaloweka mkono wangu kulifanya. Natamani iwe shauku yako pia, lakini zaidi sana kumtaka Bwana na nguvu zake kwani yeye ndo anaweza kukustahimilisha hata utakapokutana na mambo mazito katika kufanya kazi kwako. Mungu ana nguvu. Nyingi sana tena. Kutembea na Mungu na kufanya nae kazi alozokupa kufanya kwa njia ya vipawa na karama na uwezo mbalimbali ni jambo linalohitaji USHIRIKA wenye nguvu zaidi kuliko hisia za umaarufu au kutamani kuonekana. Kimsingi, ukisema wewe na Mungu mnatembea pamoja mwaka huu wa 2016 maana yake lazima muwe nay ale makubaliano na mapatano. Lazima mkubaliane kufanya kazi pamoja lakini lazima ujue kuwa wewe na Mungu hamlingani halafu pia ujue kuwa Mungu sio mjomba bali BABA. Lazima ujione tegemezi kwa BABA ambaye kimsingi ndo anaekufanya uendelee kuwepo mpaka sasa na aliyekusaidia kuvuka na kuingia mwaka huu mpya. Lazima ujue utaishi ukilifanya lile kusudi la wewe kuuona mwaka 2016 na kwakweli utaishi ulilifanya hilo tu mpaka utakapoambiwa kuondoka. Kumbuka hata kama ni kufa au Bwana Yesu kurudi ni lazima itatokea wakati wewe ukiendelea na shughuli zako za kila siku, kizuri ni kwamba kama ulikuwa unatembea na kufanya kazi na Mungu kwa moyo safi utakutwa uko na Mungu kwahiyo itakuwa njema tu.
Kama nilivosema, mwaka huu ni kutembea na kufanya kazi za Mungu pamoja nae, yaani MUNGU KWANZA. Huyu Mungu tunaetaka kutembea na kufanya kazi zake pamoja nae ni Mungu mwenye nguvu, nguzu na uwezo mkubwa kuliko dunia hii tunayoshi n ahata ulimwengu wote. Kama Simba anakutisha kwa nguvu zake sasa Mungu ndo alimpa Simba hizo nguvu kwashiyo ni sawa kusema ana nguvu zaidi yake. Kama ni mambo akiwa majini ndo anakutisha sana basi ujue kuwa aliyeweka siri ya nguvu za mambo au kiboko ni Mungu na kwahiyo yeye Mungu ana nguvu kuliko hao wote. Mungu ni mkubwa kuliko ulimwengu wote na ndo maana aliufanya na kutuweka sisi pamoja na viumbe vyote vinavyoonekana na visivyoonekana na bado yeye mwenyewe akakaa nje yake lakini ndani yetu. Huyu Mungu ndiye aliyeiumba asili lakini bado kwa asili yeye ni Mungu aliye juu yake. Huyu Mungu ndo mwenye siri juu ya kufa kwetu, yaani wengine wote wanaojiita majina yote wanayojiita bado hawana ujanja na kifo lakini yeye Mungu anamiliki kifo na kimsingi ana nguvu kuliko mauti na ndo maana alikishinda kifo.
Mungu ninaetembea na kufanya nae kazi mwaka 2016 ni Mungu ambae anatoa mvua kwa wote wasio na wenye haki. Ndo huyu aliviumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Ana nguvu sana kiasi kwamba magonjwa yanapona na ana uwezo wa kukurejeshea furaha na amani. Hata kama dunia nzima imekukataa basi huyu Mungu ana huruma na upendo wa ajabu na anakupokea bila masharti. Kutembea na Mungu wa namna hii kwa mwaka mzima, yaani kila sekunde na dakika na saa na siku na wiki na mwezi inatupasa sana na sisi tuwe kama yeye, yaani tuakisiwe na nguvu zake ili tudhihirishe utukufu wake katika maisha yetu ya kila siku kwa mwaka mzima.
Kama wewe ni mwalimu basi nguvu za Mungu zionekane katika kufundisha kwako kwa mwaka huu badala ya maneno mengi yanayoleta raha ya usingizi badala ya mabadiliko. Kama wewe unaandaa matukio basi andaa na udhihirisho wa nguvu za Mungu uwe dhahiri na usiwe na kuokoteza kana kwamba nguvu za Mungu ni kama za TANESCO. Kuandaa matamasha kusiwe tena kama sehemu ya kuburudika tu bali iwe sehemu ambayo mabadiliko ya kweli ya tabia yanatokea kwani nguvu za Mungu zipo mahali hapo. badala ya kuandaa matamasha ya mashindano basi mwaka huu andaa tamasha kwa ajili ya kumdhihirisha Mungu katika kati ya watu wanaotakiwa kuwepo hapo.
Hii yote ni kwasababu umesema unataka kutembea na Mungu, umesema unataka kuongeza ushirika na Roho Mtakatifu, umesema unataka kufanya kazi na Mungu, umesema unataka kuonaudhirisho wa nguvu za Mungu na Ufalme wake. Hii ina maanisha kuishi na kutembea chini ya mamlaka ya jina lake, pamoja na kanuni au neno lake. Kufanikiwa kwako kwa mwaka 2016 kunategemea sana KIWANGO CHAKO CHA USHIRIKA NA MUNGU, yaani unatumia muda gani kuwa na Mungu katika maombi na tafakari zako, yaani umemruhusu Mungu aathiri mfumo wako wa kufikiri na kuubadilisha kwa kiwango gani, yaani umeamua kumtanguliza Mungu katika mambo yako kila siku kwa kiwango gani, yaani unazungumza nae au umemfanya yeye kuwa kama kituo cha polisi tu?
Ni ukweli kuwa unaweza kusema unatembea na kufanya kazi na Mungu mwaka huu na huku ukijua kuwa Mungu huyo ana nguvu, cha ajabu wewe ukabaki huna hizo nguvu zake na huku uko nae. Ni muhimu sana kumtaka BWANA NA NGUVU ZAKE maana huenda safari unayopita hutaweza kushinda kwa vinguvu vyako vya soda. Ni hatari sana kujitegemea na kutengeneza mazingira ya kujiona unaweza peke yako huku ukijua kuwa hata kesho tu huna uhakika wa kuamka. Kwa hiyo, unapoendelea kutembea ndani ya UTUKUFU WA MWAKA 2016 ujue kuwa uliyeamua kutembea nae, yaani Mungu ni mwenye nguvu, yaani anamiliki nguvu na kwakweli unatakiwa na wewe kufanya mambo yako yote ukidhihirissha nguvu za Mungu ndani yako maana anaishi na kutembea pamoja na wewe.
Huenda ni biashara unafanya au ni huduma au chochote kile, basi nguvu za Mungu zionekane katik hayo yote ukijua kuwa nguvu za Mungu zinapodhihirika kwenye jambo lako huwavuta watu upande wa Mungu ambao ndo wewe upon a kwa hiyo utaanza tena safari ya kujifunza kusifiwa kwa kuwa unaonekana wewe ingawa aliyekupa kazi yuko pembeni yako. Lipo jambo kubwa sana katika kuishi na kutembea na nguvu za Mungu katika maisha yetu ya kila siku na kwa kweli huenda likawa sababu ya mambo mengi.
Kutembea na nguvu za Mungu mwaka huu kunahitaji sana pia shauku ya kila mtu, maana ukipewa nguvu usizozitaka ni wazi kuwa utazitumia vibaya. Na kwa hiyo lazima uonyeshe shauku na hamu ya kuzitaka nguvu za Mungu, na pia uelewe kuwa jambo hili la kuonyesha shauku halitakuwa jepesi sana kama unavyowaza. Hapo ipo gharama ya kulipa, maana kimsingi chochote utakacho gharamikia kukipata ni wazi kuwa hata namna utakavyokichukulia na kukitunza ni tofauti sana na kama ungedondoshewa tu. Safari hii ya shauku ya kuzitaka nguvu za Mungu inahitaji nidhamu ya hali ya juu, kutumia muda wa kutosha magotini, pia kuendelea kujikana katika mambo ambayo yanweza kukusaidia kukuondolea shauku yako. Kiukweli, kama moyo wako una shughuli nyingi ni vigumu sana kuweza kupata shauku ya kumtaka BWANA NA NGUVU ZAKE kwani kikombe kilichojaa tayari utaongeza nini juu yake. Kikombe kimejaa mchanga, hata ukiongeza maji bado kimejaa tu na hakitaweza kuongezewa kitu.
Kumbe unatakiwa ujichunguze na ujipime, ujikague na ujitafute, ujifichue na ujiambie ukweli wa moyoni kuhusu hali ya moyo wako kwani inawezekana kuwa usione udhihirisho wa nguvu za Mungu mwaka huu kwakuwa Mungu hana nafasi ndani yako. Usisahu kuwa unaweza kumkaribisha Bwana Yesu ndani yako na bado asikusaidie kwa lolote. Ukimkaribisha mgeni halafu ukamuacha sebuleni wewe ukaaenda jikoni utakuja kujikatisha tamaa sana utakapojua kuwa mgeni amefunga na muda wa kuondoka umefika. Vyovyote itakavyokuwa, jitahidi sana kumtaka Bwana na nguvu zake ili na wewe utembee katika nguvu zake, hata hivyo mwaka huu ni MUNGU KWANZA.
By Raphael JL: YKM Founder
Box 3613
Dodoma
www.ykmjesusup.org 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428