Mungu kwanza

Monday 8 July 2019

KUOA NA KUOLEWA KWA MZALIWA WA KWANZA



Kuoa au kuolewa kwa wazaliwa wa kwanza, mara nyingi kunakuwa kwa shida, au kunakuwa nje ya utaratibu mzuri, kwa kuwa tu wao ni lango na mkondo wa Mungu!

 Je, unajua mbaraka mmojawapo wa mtu kuwa mzaliwa wa kwanza kwa haki ni kupata msaada wa uongozi wa Mungu katika kuoa au kuolewa kwake?

 Hili ndilo lililotokea kwa Yakobo. Biblia inatueleza jinsi Isaka alivyokuwa anaachilia Baraka za mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo, kwa mfano, katika Mwanzo 28:6 tunasoma ya kuwa “na katika kumbariki akamwagiza, akasema, usitwae mke wa binti za kaanani”,

Unadhani ni kwa nini iwe hivyo? Ni kwa sababu mwenzi wa maisha wa mzaliwa wa kwanza anaandaliwa atumike kupitisha mtoto atakayebeba lango la haki ya mzaliwa wa kwanza.

 Naamini unakumbuka jinsi kuoa kwa Yakobo kulivyokuwa kwa matatizo na katika mazingira ya kukatisha tamaa shetani alikuwa anatafuta Yakobo asimuoe Raheli – ili kukwamisha kuzaliwa kwa Yusufu!

 Sasa unaweza ukaelewa kwa nini hali ya kukosa mtoto katika ndoa ya Ibrahimu kulileta maamuzi mabaya ya kuzaa na msichana wa kazi. Ni kwa sababu shetani alitaka Ishmaili achukue nafasi ya Isaka ya mzaliwa wa kwanza wa haki.

 Ni kweli Mungu alimwambia Ibrahimu ya kuwa “atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi” (Mwanzo 15:4). Lakini sii kwa kuzaa na mwanamke yeyote aliyemtaka yeye au kwa kushauriwa na mke wake!

 Ishmaili alitoka katika “viuno” vya Ibrahimu kwa nini basi Mungu alimkataa? Tofauti ya Ishmaili na Isaka mbele za Mungu ilikuwa ni nini, wakati wote walikuwa wametoka katika “viuno” vya Ibrahimu?

 Tofauti yake ilikuwa ni matumbo ya akina mama walio–wazaa! Mungu alimwambia Ibrahimu ubora wa tumbo la uzazi la Sara ukilinganisha na lile la Hajiri aliposema: “Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake” (Mwanzo 17:15,17).

 Sii kila tumbo la uzazi la kila mwanamke limeandaliwa kwa jinsi hii. Na kwa sababu hii sii kila mwanamke anayeolewa na kijana aliye mzaliwa wa kwanza atakuwa na uwezo wa kumzaa “Isaka”, kwa ajili ya Mungu, na kwa ajili yako!

 Tena, ni muhimu kujua ya kuwa si kila msichana atapata nafasi ya kuolewa kirahisi na “Ibrahimu”. Uwe na uhakika shetani atajitahidi kuwasukuma akina “Hajiri” kwa Ibrahimu ili kuvuruga ndoa yake!

 Na tena, ikiwa msichana umempata “Ibrahimu wako” na ukaolewa naye kwa msaada wa Mungu, usishangae ukikuta tumbo lako la uzazi likipata vita na unashindwa kuzaa!

 Naamini unaweza ukaelewa kwa nini Sara alipata shida ya kuzaa kwa Ibrahimu wake; na kwa nini Rebeka alipata shida ya kuzaa kwa Isaka wake; na kwa nini Raheli alipata shida ya kuzaa kwa Yakobo wake; na kwa nini Hana alipata shida ya kuzaa kwa Elkana wake!

 Ni ili wasiweze kupitisha wazaliwa wa kwanza wa haki ili Mungu apate kuwatumia kama lango katika kizazi kilichokuwa kinafuata baada yao. Fuatilia mwenyewe kwenye biblia ulione hili!

 Utaona ya kuwa Sara alimzaa Isaka, Rebeka alimzaa Yakobo, Raheli alimzaa Yusufu, na Hana alimzaa Samweli!

 Pia – utaelewa baada ya kukueleza hayo, Ibrahimu alipata mzigo mkubwa moyoni wa kuona ya kuwa mtoto wake Isaka anapata msaada wa Mungu katika kuoa kwake.

 Ibrahimu alimweleza mfanyakazi wake aliyemtuma kumtafutia Isaka mke ya kuwa 

“Bwana, Mungu wa mbingu aliyenitoa katika nyumba ya babaangu,… yeye atampeleka malaika wake mbele yako” (Mwanzo 24:7).

 Unadhani Ibrahimu alilijuaje hili, la kuwa Mungu wake amemtuma malaika wake kwa kazi maalumu ya kuhakikisha ya kuwa – Isaka aliyekuwa mzaliwa wake wa kwanza kwa haki anapata mke sahihi? Ni lazima Ibrahimu alikuwa anaomba juu ya kuoa kwa Isaka kwa mzigo sana, huku akijua umuhimu wa Isaka kama lango na kwa hiyo Mungu hataruhusu aoe mwanamke yeyote tu!

 Shetani aliwapiga vita sana wazaliwa wa kwanza juu ya hili kiasi kwamba anawafanya wazae watoto wao wa kwanza nje ya ndoa!

 Una mzigo wa kiasi gani moyoni mwako wa kumuombea mzaliwa wako wa kwanza – wa kiume juu ya kuoa kwake au wa kike juu ya kuolewa kwake?

 Ndiyo maana nakushauri Mungu akupe kuona umuhimu huo, na pia akupe nguvu za kumwombea ipasavyo juu ya maamuzi ya kuoa au kuolewa kwake, na/au juu ya ndoa yake!

 Mungu akubariki sana Watumie wengine Ujumbe huu!


Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428