Huwezi
kujisikia tu kuweka maji kwenye tank la gari inayotumia petrol, yaani huwezi tu
ukapenda kuweka chumvi kwenye chai na sukari kwenye mboga. Huwezi tu ukavaa
viatu mikononi hata kama unapenda sana iwe hivo, unawezaje kuvaa shati miguuni
kama suruali au gauni? Hebu fikiria kuwa umealikwa kwa ajili ya chakula, halafu
unaambiwa agiza chakula upendacho halafu wewe unaagiza chakula kwa woga
ukiogopa bei halafu mwishoni unaambiwa ulitakiwa kuagiza bila kuwa na wasiwasi
wa bei. Au wewe pata picha umekufa na ukafanikiwa kufika mbinguni, unafika tu
unaanza kuonyeshwa kila kitu ambacho ulikuwa utakiwa uwe nacho yaani kila
ulichostahili kuwa nacho. Ukaonyeshwa mumeo au mkeo, ukaonyeshwa magari ambayo
ungekuwa nayo,unaonyeshwa aina ya maisha ambayo ulitakiwa kuyaishi ukiwa
duniani, yaani unaonyeshwa kila aina ya mambo uliyokuwa unastahili kuwa nayo.
Wapo watakaolia na kuomba kurudhishwa tena duniani ili waje walipize kisasi
kwani walinga’ng’ana na mambo waliyopenda na kutamani kuwa nayo kwa gharama ya
yale waliokuwa wanastahili.
Ninachosema
hapa ni hiki, kuna utofauti mkubwa sana kati ya unachotaka na unachostahili.
Utofauti wake upo kwenye mengi lakini ni pamoja na nani anaekupa na kwa nini
anakupa maana kila kimoja kati ya hayo vina nguvu kwa namna yake katika maisha
ya mtu. Ukiingia kumuomba Mungu unaombaje, kwamba Baba akupe unachotaka tu ama
unachostahili, kumbuka mapenzi ya Mungu kwako ni zaidi ya unachotaka au
kutamani bali zaidi sana kile unachostahili. Kutokujua unachostahili ni mtego
mkubwa sana unaozaliwa na kutokujijua na kujitambua mwenyewe maana huwezi kujua
unachostahili kama hujijui. Unaweza usinielewe kama utaamua kufanya hivyo
lakini wazo la msingi hapa ni jepesi sana kueleweka. Bwana Yesu alishawahi
kusema usitoe chakula cha watoto ukampa mbwa, najua alikuwa ana maana yake kwa
mazingira yale lakini nataka tu uone kitu hapo. nataka uone kuwa kipo chakula
ambacho watoto wanastahili na mbwa wanastahili, huwezi kumpa makombo mtoto halafu
mbwa ukampa chakula freshi, lazima uwe na shida.
Changamoto
ya mambo unayotaka ni mengi ikiwemo; Unachotaka kimetokana na maisha ya makuzi,
yaani umeona na umesikia nini, ulifanyiwa nini wakati unakua, ulikwenda wapi,
ulikula nini au ulikuwa unalishwa nini, pia kila tukio lilitokea katika maisha
yako lilichangia sana kukutengenezea aina ya mahitaji ambayo yatakuwa na sauti
na nguvu kubwa kwako hivi sasa umekua.
Ndo maana utakuwa watu wanasema kuna vyakula hawezi kula, sio kwamba
vyakula hivo ni vibaya, la! Ila ikufuatilia utagundua kuwa lazima kuna
muunganiko wa kimaana sawa na mambo yaliyotokea katika maisha yake huko nyuma.
Watu wameathiriwa na makuzi yao kwa kiwango ambacho ufahamu wake ndio mpaka wa
mahitaji yake. Ngoja nikuelezee kidogo utanielewa hapo chini.
Huwezi
kumuomba Mungu akupe kitu usichokijua, kama ambavyo huwezi kuomba kitu na
hujawahi kukiona au kukikisia labda ufunuliwe au uigize kwa mtu. Mfano, umeenda
mbele ya baba yako wa mbinguni halafu anakwambia sema utakacho nikupe, wewe kwa
akili zako na ufahamu wako unamuomba akupe baiskeli, hapo sio kosa lako maana
hujawahi kuona kikubwa zaidi ya hicho. Hata kama ni gari au baiskeli bado kuna
aina nyingi sana za vitu hivyo na kwa hiyo huwezi kuomba usichokijua au
kukifahamu. Ni lazima utaomba sawa na ufahamu wako. Huu ndo msingi wa maombi
yetu mengi kwa Mungu, huwa tunaishia kuomba tunayotaka tu na kuishia hapo, au
tunayotamani na kuishia hapo na kumbe yapo tunayostahili sema tu vile hatupendi
kulipa gharama yake. Nitaelezea zaidi hapa chini.
Jambo
lolote unalostahili halitokani na maoni ya mtu au maoni yako, hapana. Weka hilo
akilini. Kama ilivyo kwa gari, kwamba inatumia mafuta ya diseli au petrol
haitokani na maoni ya mtumiaji au muuzaji bali mtengenezaji. Huwezi ukajipangia
na kujibadilishia leo ukaanza kuvuta hewa na naitrojeni na huku
aliyekutengeneza ameshakuweka oksijeni. Unachostahili ni mawazo halisi ya
mtengenezaji au muumbaji wa kitu au mtu. Kila mtengenezaji au muumbaji, moja
kati ya tabia yake ni KUKISTAHILIHILISHA kile anachokitengeneza au ile bidhaa,
yaani anakiwekea utaratibu na kanuni na faida ndani ya kanuni ili kukifanya
hicho kitu kiwe na maisha yenye maana. Gari linastahili kutembea barabarani,
samaki baharini au kwenye maji, hii huwezi kubadilisha hata kama unataka au kupenda
kwa namna gani. Weka akilini hii.
Unachosathili
unaweza ukakijua toka kwenye akili ya mtengenezaji, wengi hutumia hata vijitabu
vya maelekezo kuonyesha namna nzuri ya kutumia bidhaa fulani na usiposoma ujue
lazima utakosea tu. Kila kilichotengenezwa kina mwongozo na utaratibu wa
matumizi yake, haukitumii tu kwa hisia zao ama tu vile unavyopenda au
unavyotaka, ama sivyo kitakulipukia na ukabaki kumlaumu mtengenezaji. Mimi na
wewe pia tumeumbwa na mtengenezaji ambae ni Mungu. Mawazo yake Mungu, namna anavyotaka
sisi tuishi na kufanikiwa ameviweka katika biblia. Biblia inayafunua mawazo
halisi ya Mungu juu yetu na kila kitu kuhusu maisha. Mawazo ya Mungu katika
uumbaji wetu ndio mambo tunayotakiwa kuyajua maana ndio tutajua tunayostahili
badala ya kukesha na tunayotaka tu.
Mtu
yeyote mwenye akili timamu anajua kuwa ukipewa uchague kati ya unachotaka na
unachostahili atachagua anachostahili maana hicho ndo ukamilifu wake. Unachostahili
kina nguvu kubwa sana maana kimefungwa ndani ya hatma yako. Ukikipata unachostahili
katika kila hatua ya maisha yako utaanza kuona utofauti wa kuishi maisha ya
kubahatisha. Hebu wewe mwenyewe fikiria, upate kazi unayostahili, sio tu kwenda
kusomea kozi kwakuwa utapata mkopo, fikiri upate mke au mume unaestahili badala
ya kujaribu jaribu kama nguo za Mtumba grade X, fikiria upate kila
unachostahili itakuwaje? Ni kweli kwamba vitu vyote ni halali lakini si vyote
vinafaa au vinajenga, na hapo ndo utaelewa vizuri kuwa unachostahili ni sehemu
ya maisha yako. Wewe endelea kuingia kwenye maombi na ubabe wako wa kijinga na
kumuomba Mungu mambo unayotaka na huku unayo mengi sana unayostahili na yako
pembeni. Unaomba mkokoteni na ulistahili kumiliki ndege binafsi (ACHA UJINGA),
acha kula makombo na chakula freshi kiko menzani, kwani una haraka ya nini?
Yaweke haya akilini mwako maana yatakufaa. Wewe jiulize tu hata sasa, makosa
mangapi umefanya kwa kulazimisha mambo unayotaka tu?
Ngoja
nikukumbushe, aina ya maombi ya mtu anaejua nini anastahili ni kama yale
aliyoomba Bwana Yesu, akasema BABA KIKOMBE HIKI KINIEPUKE LAKINI SI KAMA
NITAKAVYO MIMI BALI MAPENZI YAKO YATIMIZWE AU KAMA UTAKAVYO WEWE. Kwenye kila
uombalo au ufanyalo jifunze kuacha nafasi ya Mungu na mapenzi yake kutimia ili
upate unachostahili hata kama ni kigumu. Huu ndo ukweli kwamba kuomba mapenzi
ya Mungu kutimia maishani mwetu ndio kiwango cha juu na cha mwisho cha kupata
unachostahili maana Mungu hawezi
kukufanyia hila na huku yeye mwenyewe amesema ANAKUWAZIA MEMA. Ile kujua tu
kuwa Mungu anakuwazia mema inatosha kukufanya utulie na uache kuhangaika maana
umeshapewa uhakika na aliyekuumba na kukutengeneza kuwa anakuwazia mema na kwa
hiyo chochote kitokacho kwake lazima kiwe kizuri na kinachokufaa wewe.
Ukweli
ni kwamba kujua unachostahili ni moja kati ya suluhisho ya matatizo mengi sana
maana inaleta utulivu wa ndani na uhakika way ale tunayohitaji. Ukijua
unachostahili hutakuwa tayari kushusha bei maana unajua thamani yako. Ukijua
unachostahili hutahangaika na makombo, uikjua unachostahili hutapoteza muda
kutembea kwa miguu na huku magari ya moto yamepaki kwenu. Ukijua unachostahili
hutadanganyika na vitu vya dunia hii na huku unajua hazina yako iko wapi.
Ukijua unachostahili hutawapa mbwa chakula cha mumeo au mkeo(ACHA UJINGA WEWE).
Ukijua unachostahili hutakaa na wapiga majungu na huku kinywa chako kimejaa
neema na baraka. Kujua unachostahili ni ishara ya juu kabisa ya kujitambua
katika Mungu maana yeye Mungu ndio uhalisia wa sisi ni akina nani.
Haya
sasa, anza leo kubadilisha kuomba kwako, ukiomba unayotaka na kutamani malizia
na unayostahili na kukazia kwenye hayo maana kila zawadi nzuri hutoka kwa baba
wa mianga. Usisahau kusema, MAPENZI YAKO YATIMIZWE KWANGU KAMA YANAVYOTIMIZWA
HUKO MBINGUNI, usisahau kusema SI KAMA NITAKAVYO MIMI BALI KAMA UTAKAVYO WEWE.
Maombi yaliyojengwa katika ubinafsi wa unachotaka tu yatakuchosha, utajiona
umeomba sana kuliko ubora na kiwango cha majibu halafu utaanza kuchukia maombi
na kuacha kabisa kuomba. Huna cha kupoteza kama utapoea na kupotelea ndani ya
mapenzi ya Mungu. Uwe na siku njema. Jesus Up!
YKM JESUS UP 2019
0 comments:
Post a Comment