Mungu kwanza

Monday 23 November 2020

KIZAZI CHA KUJITOA MUHANGA

KIZAZI CHA KUJITOA MUHANGA BILA KUJUA KINAJITOA MUHANGA.

Kuamua kuficha umri, kabila, elimu na huku huwezi kuficha sehemu zako za siri yaani kila mwanaume/mwanamke anaziona huko nako ni kujitoa muhanga.

Kuamua kuishi kwa gari ya mkopo ya kutembelea na hauna ajira wala biashara inayokuingizia kipato, na upo chumba cha kupanga na hutaki hata rafiki zako wakaribu wajue unaishi wapi; huko nako ni kujitoa muhanga.

Unafanya kazi kwa ndugu yako halafu unamuibia ukiamini kufanya hivyo ni ujanja na unajijenga; hujui unachofanya ni sawa na kukata tawi ulilolikalia ukiamini likikatika wewe utakuwa salama huko nako ni kujitoa muhanga.

Ulikuwa na rangi nzuri, rangi asilia ukaamua kujikoboa. Kama huko sio kujitoa muhanga ni nini? Maana mwili umekuwa kama 'tetracycline' rangi mbili. Kama wewe ni punda hata ukijipaka rangi za mistari myeusi na myeupe huwi pundamilia.

Unajua kabisa unampenda ila hujiongezi, anasubiria useme neno wewe ndio kwanza unamwita dada. Anakuja mtu anasema neno na anaoa halafu unagoma kumuita huyo jamaa shemeji. Unaanza kulalamika kuwa amekubebea mke wako khaaah huko nako ni kujitoa muhanga. Kama Mungu alitamka liwe anga na likawa basi nawe usiogope kusema uwe mke.

Kulala saa mbili usiku na kuamka saa mbili asubuhi kila siku huko nako ni kujitoa muhanga. Kuna kulala kunakoletwa na uvivu-huku ndio mtu anagalagala kitandani na usingizi hauji. Halafu kuna kulala kwa sababu umechoka baada ya kufanya kazi-huku huwa kunaleta usingizi haraka na baada ya muda usingizi unaisha, unakata na mlalaji huishia kusema leo nimelala sana.

Hajakuoa anakupiga makofi mbele za watu na bado unamng'ang'ania, unaambiwa hakufai unaishia kusema hamjui tu anavyonipenda atabadilika tu. Ni kweli hawajui ila wanaona unavyojitoa muhanga. Simba hata ukimnyoa manyoya hawi paka kisa umempa na maziwa.

#Kuna nguvu hutumiwa vibaya#

JIPIGE PANAPOUMA

Mwl Makwaya
Kuwa Ni Kufanya.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Contact

P.o.Box 1404 Mwanza Tanzania
E-mail : frhebron@yahoo.com , frhebron@hotmail.com
Mobile: +255716 423 428 , +255766 710 028

Website Visitors

Copyright © Hebron Fredrick All Rights Reserved Designed and Developed by Hebron Fredrick+255716 423 428